Mkurugenzi Manispaa Morogoro atoa shukrani kwa Meya kwa kuikabidhi Manispaa ndoo za kunawia maji katika kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba (kulia), akimkabidhi Mkuu wa Masijala ndoo na sabuni iliyotolewa na Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga. |
MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amempongeza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, kwa kujali afya za Watumishi baada ya kuikabidhi ndoo za kunawia maji pamoja na sabuni katika mapambano ya Virusi vya Ugonjwa wa CORONA.
Akizungumza Ofisini kwake leo Machi 30,2020 , mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, amesema ni wakati wa Viongozi kuangalia namna ya kuwajali wananchi wao na kuendelea kutoa elimu katika kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
"Tunamshukuru sana Mhe. Meya wetu wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, kwa hiki kidogo alichotoa kwetu ni kikubwa sana kwani ameonesha ni kwa namna gani anajali afya za Watumishi wake kama Kiongozi wa Manispaa hii, pia Manispaa yetu tumebahatika kupata Baraza bora la Madiwani jambo ambalo ni la kujipongeza hususani katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa CORONA, hivyo basi kwa niaba ya Watumishi wote wa Manispaa tunasema asante Mwenyezi Mungu akambariki na kumuongezea alichotoa " Amesema Sheilla.
Katika hatua nyengine, amechukua nafasi ya kuwakumbusha Wananchi, Wafanyabiashara, Bodaboda, Bajaji, Vituo vya Mabasi, Wamachinga pamoja na maeneo yote yenye mikusanyiko waendelee kuchukua tahadhari ya kujikinga na Ugonjwa huo ikiwemo kunawa maji tirirka na sabuni pamoja na kutumia vitakasa mikono ili kujiweka kwenye usalama.
Amesema kuwa huu ni wakati wa kuhakikisha hakuna mikusanyiko isiyo ya kilazima, huku akitoa wito kwa Watendaji wote kuanzia ngazi za Mitaa pamoja na Kata kuhakikisha wananchi wanazingatia maagizo yanayotolewa na Viongozi wa Ngazi za Juu pamoja na Wataalamu wa afya na kwa wale watakaokuwa wakaidi wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Post a Comment