MANISPAA YA MOROGORO YAWATOA HOFU WANANCHI UPATIKANAJI WA VIBALI VYA UJENZI.
Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Morogoro, Emeline Kihunrwa, akizungumza na Watendaji wa Kata na Mitaa kuhusu elimu ya upatikanaji wa Vibali vya Ujenzi kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Morogoro. |
MANISPAA ya Morogoro imewatoa hofu Wananchi kuhusiana na
suala zima la upatikanaji wa Vibali vya Ujenzi katika maeneo ya Kata zao.
Hayo yamezungumzwa leo Machi 26 , 2020 na Afisa Mipango Miji
wa Manispaa ya Morogoro, Emeline Kihunrwa ,katika mkutano na Watendaji wa Kata
pamoja na wa Mitaa katika majadiliano ya jinsi ya kutoa elimu kwa Wananchi juu
ya Vibali vya Ujenzi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema kumekuwa na
taharuki kwa baadhi ya Wananchi juu ya kutopata Vibali vya Ujenzi wakati tayari
wameshaomba vibali hivyo.
Amesema kuwa Vibali vya Ujenzi havitolewi kiholela bali zipo
taratibu zinazotumika katika upatikanaji wa Vibali hivyo.
Aidha amesema kuwa maeneo yanayostahili kupewa vibali vya
Ujenzi ni yale ambayo yamepitiwa na zoezi la urasilimishaji wa Ramani za mipango Miji.
Amesema zaidi ya asilimia 60 hadi 80 ya makazi mengi
yaliyopo Mijini yamejengwa kiholela bila ya kuzingatia Ramani za Mipango Miji
na maeneo mengine hayajapimwa lakini yamejengwa jambo ambalo ni kinyume na
Sheria.
“ Sisi sio kwamba tunakataa kutoa Vibali vya Ujenzi, mkumbuke hivi
karibuni Waziri Mwenye dhamana katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, alisimamisha
zoezi la utoaji wa Vibali hadi pale Serikali itakapotoa miongozo mipya hii ni
kutokana kuwa yapo maeneo ambayo hayajapimwa na mengine ni hatarishi hivyo
tukiwa tunatoa vibali kiholela itatuletea shida upande wetu na kuongeza
Migogoro isiyo na tija, niwaombe Wananchi wa Manispaa ya Morogoro tuwe
wavumilivu lakini wale wadanganyifu waache tabia zao unakuta mtu nawasilisha Ramani Mipango Miji lakini anachokwenda kukijenga kinakuwa tofauti watu wa
namna hii kwakweri tutakula nao sahani moja” Amesema Emeline.
Hata hivyo amesema kuwa, kibali cha Ujenzi (Building Permit)
ni nyaraka ya Kisheria inayotolewa na Mamlaka za Upangaji (Planning
Authorities) ambazo ni Mamlaka za Serikali za Mitaa (The Local Government
Authorities) ili kuruhusu Ujenzi mpya, kubomoa, kuondosha, kuongeza, au kufanya
marekebisho makubwa.
Kwa upande wa Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Eng. Juma
Gwisu, amesema moja ya faida ya kibali cha Ujenzi ni pamoja na kurekebisha
kasoro zinazoweza kuathiri uimara wa jengo na mifumo mingine ya maji safi na
taka, tahadhari za moto, umeme, usalama wa jamii na uharibifu au uchafuzi wa
mazingira pamoja na kupisha miundombinu inayotakiwa kupita kwa jamii kutoakana
na ujenzi unaofuata vipimo maana nyumba zikikosa vipimo hata kuendeleza huduma
za Kijamii inakuwa ngumu kutokana na ufinyu wa maeneo yaliyojengwa bila
mpangilio.
“Niwaombe Watendaji nyie muwe mabalozi wa kusimamia suala
hili, tuanataka Miji yetu ipangike, sio tu kuhimiza Vibali hivi ili Manispaa
tupate fedha lakini tunachotaka sisi ni kuona Wananchi wetu wanaishi katika
makazi bora na imara yasiyokuwa na uhatarishi wa maisha ya watu, tupate maeneo
ambayo hata tukisema tunapitisha huduma za kijamii inakuwa rahisi na ndio maana
tunasisitizia sana Vibali vya Ujenzi, maeneo kama Mkundi, Bigwa , Chamwino na
Kihonda yapo katika hali nzuri na tayari urasimishaji ushafanyika kilichobakia
ni vibali tu lakini zoezi la ugawaji Vibali vya Ujenzi tutavitoa kwa maeneo
ambayo Ramani zao zimepitiwa na Mipango Miji tna yale maeneo ambayo yameshapimwa au kupitiwa na urasimishaji ”Amesema Eng. Gwisu.
Aidha, amesema kuwa kabla ya kutoa tangazo la Vibali vya
Ujenzi vilikuwa vikitolewa kwa Shilingi 30,000/= lakini baada ya tangazo
wakaanza kutoa kwa Shilingi 45,000/= kwa maeneo ambayo hayajapimwa ambapo kwa
sasa wamesitisha zoezi hilo hadi pale miongozo itakapotoka upya na kwa maeneo
yaliyopimwa ni Shilingi 65,000/= ambapo Ramani zake zimepitia Mipango Miji na
maeneno hayo yamerasimishwa.
Pia Eng. Gwisu, amewatahadharisha Watendaji kuwa makini na watu wanaopata Vibali
kwa kutumia Ramani isiyopitishwa na Mipango Miji kwani ramani ambazo
zinapitishwa na mipango Miji nyuma zina mhuri wa Moto wa Manispaa.
Hata hivyo, Gwisu,
amesema kuwa kuchelewa kwa Vibali vya Ujenzi inasaidia sana kudhiti uendelezaji
holela Mijini na Vijijini usiozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
Kwa upande wa Afisa Utumishi Manispaa ya Morogoro, Waziri
Kombo, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi
wa Manispaa, amewaagiza Watendaji kutoa taarifa kila mwezi katika Kata
zao na Mitaa yao juu ya Vibali vya Ujenzi na kuwaripoti wale wote wanaokwenda
kinyume na tarabu za Ujenzi na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria
ikiwamo kuwabomolea nyumba zao na kushika faini au vyote kwa pamoja.
“Watendaji muwe mnatusaidia wakati mkiwa katika pitapita
zenu huko mkiona mtu kaanza ujenzi mtoe taarifa ikiwezekana muanze kumuuliza
awaoneshe kibali chake kama amezingatia sheria au mkikaa kimya sisi hatuwezi
kujua sana na mwisho wa siku tunatengeneza migogoro kwa wananchi “Amesema
Kombo.
Pia amesema Serikali ilishatamka kwamba hairuhusiwi
kuingiza Kampuni Mpya ya Urasimishaji hadi hadi pale itakapotoa miongozo Mipya , hivyo
amewaomba Wananchi kuwa na subira kwani Vibali vitatolewa kwa kuzingatia
kanuni, Sheria na Taratibu.
Katika hatua nyengine, Kombo, amewataka Watumishi na
Watendaji wote kuzingatia kanuni, Sheria na Taratibu za kazi kwani wanatakiwa
kuwahi kazini kwa muda wa Serikali uliopangwa.
Amesema suala la kulimana barua sio jambo jema sana kwani
linapunguza sifa za wafanyakazi na athari yake ni kubwa sana ikiwamo kufukuzwa
kazi , kushushwa cheo au kupigwa faini ya kukatwa mashahara asilimia 50.
Post a Comment