Header Ads

JAMII YATAKIWA KUPIGA VITA VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO

JAMII imetakiwa kupiga vita vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Hayo yamesema na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo Ole Paul,Novemba 27/2023  kwenye uzinduzi wa Mafunzo ya upigaji vita vitendo vya unyanyasaji wa Kijinsia chini ya Wajumbe wa MTAKUWWA yaliyoandaliwa na Kanisa la KKKT Dayosisi ya Morogoro yenye lengo la kuwajengea uwezo wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuifikia jamii na kutokomeza ukatili wa kijinsia.  

Akizungumza na Wajumbe wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Askofu Mameo, amesema kuwa watoto wana haki ya kupata elimu, pia wana hakai ya kutonyanyasika na endapo wataona vitendo vyovyote vinavyopelekea kuvunja haki zao , wachukue hatua mapema ya kutoa taarifa Polisi ama kwa Serikali za Mitaa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

"Jamii inapaswa kutoa ushirikiano pindi wanapobaini vitendo vya uvunjwaji haki za watoto na wanawake na waondokane na dhana iliyozoeleka ya kumtenga mtu anayetoa ushahidi ama kuripoti juu ya matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu, wanawake  na watoto " Amesema Askofu Mameo.

Askofu Mameo, amesisitiza juu ya haki ya kurithi kwa wanawake na watoto wanaoachwa baada ya wapendwa wao kufariki kuwa wana haki ya kusimamia mirathi na kurithi na waondokane na dhana iliyojengeka kuwa mtoto wa kike hana haki ya kurithi.

Kaimu Afisa Maendelo ya jamii Manispaa ya Morogoro, Josephine Mkuli, amesema kuwa, kwa sasa jamii inapata taarifa kuhusu ukatili wa kijinsia na wako tayari kuonyesha ushirikiano kwa kuibua zaidi matukio ambayo jamii inayaficha.

Naye  Mkurugenzi wa Kituo cha Kimbilio, Bi . Thabitha Kilatu, ameiomba Serikali kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaobainika kujihusisha na vitendo vya ukatili.

Kwa upande Afisa Ustawi Manispaa ya Morogoro, Sidina Mathias, amesema jamii iendelee kupewa elimu juu ya aina mbalimbali za ukatili na wapi waripoti wanapoona vitendo hivyo.

Naye mwezeshaji wa mfunzo hayo kutoka Ofisi ya Ustawi Manispaa ya Morogoro, Judith Mbelwa, ameweka wazi kuwa, mabadiliko yanaanza na mtu mmoja mmoja hivyo ni jukumu la kila mzazi kujitathimini na kama yeye mwenyewe ndiye chanzo cha kusababisha ukatili wa kijinsia badala ya kuitupia lawama jamii inayomzunguka.

Mtoa maada kutoka Kituo cha Masaada wa Kisheria Ofisi ya Morogoro Paralegal , Chediel Senzighe, amewaomba Wajumbe wa MTAKUWWA kubuni mbinu mpya za kukabiliana na ukatili wa kijinsia ili kupunguza ongezeko la vitendo vya kikatili wa kijinsia vinavyotendeka katika jamii.

Senzighe, amefafanua kuwa suala la ukatili wa kijinsia ni mtambuka hivyo Serikali yenyewe haiwezi kumaliza tatizo hilo bila kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali ili kuifikia jamii kwa urahisi zaidi kwa kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia yanaleta madhara makubwa katika kizazi kijacho.

“Ni imani yangu kuwa asasi zisizo za kiserikali kwa kushirikiana na Serikali zikifanya kazi kwa kushirikiana zitaleta mabadiliko chanya na kuisadia jamii kuepukana na ukatili wa kijinsia”. Amesema Senzighe.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.