Header Ads

JAMII INA NAFASI KUTOKOMEZA UKIMWI-RC MALIMA AKIFUNGUA MAADHIMISHO YA UKIMWI KITAIFA MKOANI MOROGORO



MKUU wa Mkoa wa Morogoro,Mhe. Adam Malima,  amesema  Jamii na Mashirika yasiyo ya Kiserikali , asasi za kiraia na wanaharakati  kuwa na juhudi endelevu za pamoja ambazo zitakuwa muarobaini  wa kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Kauli hiyo,ameitoa katika uzinduzi rasmi wa wiki ya maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ukimwi Duniani 2023 kwenye Uwanja wa Shule ya Morogoro Sekondari Mkoani Morogoro Novemba 24/2023.

"Hali ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa sasa sio nzuri hivyo  jamii kuendelea kupiga vita maambukizi mapya, nina imani na jamii, jamii zinaleta mabadiliko, jamii ndio matumaini yetu makubwa ya kutokomeza Ukimwi, kwa sababu jamii zimepambana dhidi ya HIV tangu mwanzo mwa mwaka 1988 hadi leo," Amesema RC Malima.

Katika hatua nyengine, RC Malima,  amesisitiza zaidi vijana wa kike kuhakikisha wanabadili tabia, lakini pia kujenga ujasiri wa kujiamini na kuwa na uwezo kusema hapana, pale inabobidi, ili kujikinga na maambuziki ya VVU.

“Tunaomba mashirika na wadau wa kudhibiti Ukimwi kuangalia sana katika eneo hili la kuelimisha vijana, lakini na kupeleka zile huduma rafiki kwa vijana,”Ameongeza RC Malima.

Amesema kwa tathimini ya matokeo ya utafiti miaka 2 iliyopita mwaka 2021 waliopima ni 226213 na mwaka 2022 waliopima 292000 na januari hadi Septemba  2023 waliopima ni 11620 ambapo kinachosubiriwa ni tafiti ya mwaka 2023  ili kuona hali ikoje na kuendelea kujitathimini.

Pia, amesema jukumu la kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi sio jukumu la Serikali, hivyo ameziomba Taasisi za Kidini , Nyumba za ibada pamoja na waandishi wa habari kupaza sauti juu ya kudhibiti maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.

RC Malima, amesema Mkoa wa Morogoro una jumla ya vituo vya afya vya kuzuia maambukizi ya Ukimwi kwa Mtoto kutoka kwa mama vituo 378 , hivyo Serikali itaendelea kuboresha vituo hivyo.

Mwisho amewaomba wananchi kupitia kwenye mabanda ya maonesho ambayo mwisho wake ni tarehe 1/12/2023 ambapo mgeni rasmi katika Kilele cha maadhimisho ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassimu Majaliwa Majaliwa.

Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Dkt. Ali Mussa Ali,  amezisisitiza asasi za kiraia zinazohusika na mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi    zinasimamia  kikamilifu ili kuhakikisha  Mkoa wa Morogoro  Ukimwi unapungua.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.