MBUNGE MZERU KUFANIKISHA UJENZI UZIO WA SHULE YA SEKONDARI LUPANGA, AANZA NA 500000 KAMA SEHEMU YA KIANZIO
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro Mhe. Norah Mzeru, ameahidi kufanikisha ujenzi wa uzio wa Shule ya Sekondari Lupanga Manispaa ya Morogoro lengo la kuongeza ulinzi kwa wanafunzi na mali za shule.
Mhe. Mzeru, ameyasema hayo Novemba 07/2023 wakati wa hafla ya mahafali ya kidato cha IV shuleni hapo kufuatia maombi yaliyowasilishwa na wanafunzi kupitia risala iliyosomwa mbele yake.
“Nataka niwahakikishie kwamba tutajenga uzio hapa na mwakani mkija hapa mtaona mabadiliko ombi langu kwanza muanze wenyewe na mimi nachangia laki 5 kama kianzio kwenu harafu pale ambapo mtakapoishia mniambie nimalizie dhumuni letu la uzio huu ni kwa ajili ya usalama wa wanafunzi na mali zote zilizopo shuleni" Amesema Mhe. Mzeru.
Aidha, Mhe. Mzeru ,ameishukuru serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuingiza kiasi cha Milioni 5 ya miradi ya maendeleo katika Kata hii pamoja na ujenzi wa madarasa mapya ambayo yatasaidia sana kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa.
Naye Diwani wa Kata ya Kilakala , Mhe. Marco Kanga, amesema Mkuu wa Shule amekuwa akipambana kwani alivyoingia madarakani mwaka 2020 akiwa na mkuu huyo walikuta Lupanga ina madarasa 10 na leo Lupanga ina jumla ya madarasa 23 ambapo ni maendeleo makubwa chini ya Uongozi wa Mwalimu huyo.
"Mkuu wa Shule hapa Lupanga Dada yangu Ndunguru anafanya kazi kubwa sana, tulikuta shule hii madarasa 10 tukaongeza yakawa 23 , lakini Waalimu walikuwa wanachangia vyoo na wanafunzi lakini leo Waalimu wana vyoo vyao na wanafunzi wana vyoo vyao,huduma ya maji ipo na ufaulu uliongezeka na hata hawa wanafunzi 100 waliotajwa waliofaulu kujiunga na kidato cha 5 na vyuo mbalimbali ni matunda yetu ya BMK kushirikiana na wadau wa elimu na Uongozi wa Shule, hii ni hatua kubwa inaonesha ni jinsi gani Mkuu huyu yupo siliazi na kazi zake na ni mfano wa kuigwa "Amesema Mhe. Kanga.
"Mhe. Mzeru Mwalimu huyu kwa kushirikiana na waalimu wenzake wanafanya kazi kubwa sana, tunatambua mchango wako Mbunge wetu Viti Maalum, hata ukiangalia taswira ya mbele ya madarasa ya shule hii imetokana na mchango wako , endeleeni kutesemea huko juu kuna fedha zinatoka Serikali Kuu na fedha zinatoka mapato ya ndani, fedha hizi za Serikali Kuu nyie Wabunge ikiwemo na Mbunge wetu wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Dkt. Abdulaaziz Abood , ndio mnapambana kuhakikisha fedha hizi zinakuja katika Halamshauri yetu" Ameongeza Mhe. Kanga.
Akitoa maelezo ya awali Mkuu wa Shule ya Sekondari Lupanga, Mwal. Flora Ndunguru , amebainisha mikakati ya kitaaluma ambayo shule imejiwekea ikiwa ni kuhakikisha wanaendelea kukuza taaluma na kufundisha kwa bidii ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wananafanya vizuri katika mitihani ya Taifa na hivyo kuijengea sifa Manispaa ya Morogoro na mkoa kwa ujumla.
Mwal. Ndunguru, amempongeza Mbunge Mzeru kwani amekuwa msaada mkubwa katika Shule hiyo ambapo katika msaada wake wa kuona shule inakuwa na mazingira mazuri aliweza kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ukarabati wa madarasa chakavu.
Ndunguru, amesema wanafunzi wa kidato cha nne wanaotarajia kufanya mtihani wa Taifa ni 250 ambapo wasichana 118 na wavulana 132.
Katika Mahafali hiyo Mhe. Mzeru alifanya harambee ya chagizo kwa ajili ya ujenzi wa uzio na kuweza kufanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi laki 5 kutoka kwa wazazi na wadau wa maendeleo huku laki 5 nyengine ikiwa ni ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu .
Ikumbukwe kuwa Mitihani ya Taifa ya kidato cha Nne hapa nchini kwa mwaka 2023 inatarajiwa kuanza 13/11/2023.
Post a Comment