DIWANI SULTAN AREA APIGA MARUFUKU ''VIGODORO'' KUFANYIKA MITAANI.
DIWANI wa Kata ya Sultan Area Manispaa ya Morogoro Mhe. Peter Dhahabu (Chebo),amepiga marufuku ngoma zinazovunja maadili ya mtanzania zijulikanazo kwa jina la " VIGODORO" maarufu kama Kanga Moko na kusimamisha ngoma hizo kufanyika mitaani kwenye Kata yake wakati wa usiku hali inayochangia kuharibu utamaduni wa Mtanzania na kuchochea vitendo vya ngono nyakati za usiku.
Kauli hiyo,ameitoa Novemba 17/2023 Mtaa wa Umbunga katika Mkutano wa hadhara wa Wananchi wa Kata wa kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi chake cha miaka 3 tangia aingie madarakani 2020-2023.
"Nikiwa Diwani wa Kata hii kwa kushirikiana na Chama changu cha CCM na Uongozi wangu wa Kata tumepiga marufuku vigodoro , kwani ngoma hizi ambazo huchezwa usiku kuchwa zimekuwa zikipelekea vitendo viovu ikiwemo vitendo vya ngono hali inayochangia ukiukwaji wa maadili ya Mtanzania, kama 2025 mtaninyima kura kwa kuwa nimekataza vigodoro hakuna shida bora nikose hizo kura kuliko kusema nalinda kura nikiruhusu ngoma hizi ili hali wananchi wangu na watoto wanaangamia nakupelekea Mmong'onyoko wa maadili "Amesema Chebo
Amesema ngoma hizo awali zilikuwa zimeshamiri sana katika Mitaa hali inayopelekea kuwepo kwa vitendo vya ngono ambavyo husababisha maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na baadhi ya washiriki wa ngoma hizo kujihusisha na vitendo vya ngono isiyo salama.
Aidha, amesema katika ngoma hizo kumekuwa ikiwahusisha vijana wadogo ambao hujihusisha na vitendo vya ngono pindi ngoma hizo zinapochezwa nyakati za usiku hali inayovunja utamaduni wa mtanzania pamoja na maadili ya Mtanzania.
"Ngoma hizi zimekuwa zikiwahusisha hasa vijana wadogo ambao wapo katika umri wa kwenda shule hali inayochangia mmong'onyoko wa maadili kwa vijana hawa na pia kujiingiza katika vitendo viovu vya ngono na hata maambukizi ya virusi vya Ukimwi"Ameongeza Chebo
Mwisho, ameitaka Ofisi ya Mtendaji kutoa vibali vyote vya sherehe lakini sherehe za nyumbani mwisho ziwe saa 12 jioni kwa mujibu wa sheria ili kutoruhusu ngoma hizi za vigodoro ambazo zinapelekea hata watu kuchinjana kwa ajili ya vurugu ambazo ni hatarishi wa usalama wa wananchi.
Post a Comment