Header Ads

WANANCHI WATAKIWA KUJIUNGA KWENYE MFUKO WA AFYA YA JAMII.




WANANCHI wa Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro wametakiwa kujiunga kwenye mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa (ICHF) ambao ni mpango wa uchangiaji wa hiari wa huduma za afya kabla ya kuugua ili kuiwezesha familia kutibiwa kwa gharama ya shilingi elfu 30 kwa  mwaka mmoja.

Kauli hiyo, imetolewa na Diwani wa kata ya Mafiga Mhe Thomas Butabile ,  Mtaa wa Majumba Saba, katika mwendelezo wake wa ziara ya kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi cha miaka 3 akiwa madarakani 2020-2023.

Butabile, amewataka wananchi kukata Bima kabla ya kuugua ili wapatapo maradhi waweze kutibiwa bila kuchangia pesa nyingine.

 "Bima hii ni rahisi sana kwa uchumi wetu, bima hii hukatwa kwa shilingi 30000/= kwa watu  wasiozidi 6, kipaumbele cha Serikali awamu ya sita (6) inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutatua changamoto za afya, kuhakikisha uwepo wa dawa, uwepo wa wataalam, vitendea kazi na vitendanishi hivyo basi tukate bima mapema kwani ugonjwa haupigi hodi”Amesema Butabile.

Aidha, Butabile, amesema  kuwa iwapo kaya ya watu 6 au chini ya idadi hiyo watajiunga katika mfuko huo wana uwezo wa kutibiwa katika Zahanati, kiyuo cha Afya, Hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Mkoa kwa rufaa maalum kutoka katika kituo husika.

Hata hivyo, Butabile, amewataka wananchi kufuga mifugo, kama kuku, mbuzi, kondoo, bata na ngombe wakiuza ziwasaidie kujiunga kwenye Bima ya Afya iliyoboreshwa( ICHF) kwa kuwa ugonjwa haupigi hodi mtu anaweza akaugua halafu akawa hana pesa ya kwenda Hospitali.

Katika hatua nyengine, Mhe. Butabile, amewataka vijana wa boda boda kuhifadhi kiasi cha shilingi mia tano (500) kila siku ambapo ndani ya siku 60 itawasaidia kupata fedha kiasi cha shilingi 30,000 kitakachowawezesha kujiunga kwenye mfuko wa ICHF.

“ Afya ni mtaji ndio maana wote tuko hapa leo, mfuko huo ni mali yetu, ni kapu linaloratibu huduma za afya hivyo tuungalie kwa jicho pana ewe, baba mama, kijana jiunge kwenye mfuko huu mapema ili uweze kutibiwa bila usumbufu”Ameongeza Mhe. Butabile.

Naye Mtendaji wa Kata ya Mafiga, Bi. Amina Said, amesema kuwa ,  mpango wa kumsajili Mwanachama wa Bima hufanyika kwenye ofisi ya Mtendaji wa Kata  kwa kutumia teknolojia ya simu ambayo imemuondolea gharama ya kupiga picha mwanachama pamoja na usumbufu wa kuifuata huduma mbali na anapoishi.

Amina, amesema  kiwango cha kulipia Mratibu huyo wa CHF amesema ni shilingi elfu thelethini  (30,0000) kwa Mwaka Mzima kwa kaya yenye watu wasiozidi sita(6) yaani baba, mama na watoto(wategemezi) wenye umri chini ya miaka 18.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.