Header Ads

DIWANI MBILINYI AELEZEA MAFANIKIO MAKUBWA NDANI YA MIAKA 3 KATA YA LUKOBE


DIWANI wa Kata ya Lukobe, Mhe. Selestin Mbilinyi, amesema katika kipindi cha miaka 3 akiwa madarakani Kata ya Lukobe imekuwa na mafanikio makubwa sana ukilinganisha na kipindi cha nyuma.

Hayo ameyasema Novemba 19/2023 kwenye Mkutano wa hadhara wa wananchi Mtaa wa Majengo Mapya Maduka 10 wenye lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2023kwa wananchi  akiwa Madarakani.

Mhe.Mbilinyi,amesema kuwa katika kipindi cha miaka iliyopita Kata ya Lukobe haikuwa na huduma za afya lakini kwa sasa Kata hiyo ina kituo cha afya Lukobe ambacho mwishoni mwa mwezi huu mwaka 2023  kitaanza  kufanya kazi.

"Nampongeza Mama yetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tulipokea milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha afya, na sasa majengo yote muhimu yamekamilika tunachosubiria ni vifaa vya samani na vifaa tiba ili Kituo chetu kianze kutoa huduma, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila bila kumshukuru Mbunge wetu wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Dkt. Abdulaaziz Abood, kwa kukipa Kituo chetu gari la huduma za wagonjwa (Ambulance) " Amesema Mhe. Mbilinyi.

Kwenye upande wa elimu, amesema Kata ya Lukobe haikuwa na Shule ya Sekondari lakini kwa sasa Kata hiyo ina shule mpya ya Sekondari.

"Nilipongeze Baraza letu la Madiwani na Menejimenti ya Manispaa kwa kupitisha ujenzi wa Shule yetu ya Sekondari, mwanzo wanafunzi wetu walikuwa wanasafiri umbali mrefu kufuata huduma lakini kwa sasa tunashukuru Shule ipo karibu na wanafunzi wetu wanasoma , lakini Mhe. Mbunge naye tunampongeza kwa kuimarisha huduma ya Tehama kwa kutuletea Kompyuta 6 ambazo zitasaidia wanafunzi wetu kujifunza Teknolojia ya Habari " Ameongeza Mhe. Mbilinyi.

Katika upande wa shule za msingi, amesema Kata hiyo imeongeza shule 1 mpya ya Juhudi na shule hiyo tayari imeshaanza kufanya kazi wanafunzi wanasoma.

Mhe. Mbilinyi,amesema katika kuimarisha ulinzi na usalama,Kata ya Lukobe kwa sasa imeshajenga boma la Kituo cha Polisi ambacho kinasubiriwa kupata fedha kwa ajili ya umaliziaji ili kusogeza huduma ya ulinzi kwa jamii.

Aidha, kuhusu usafiri, tayari ameshawasilisha taarifa hiyo Manispaa pamoja na TARURA ambapo kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kuona namna ya kuboresha miundombinu hiyo ili kuboresha suala la usafirishaji ambalo ni changamoto ya muda mrefu katika Kata hiyo.

Amesema Manispaa ya Morogoro kwa kuona kadhia hiyo, imetenga milioni 700 mwaka fedha 2023/2024 kwa ajili ya ununuzi wa Greda ambalo litatumika katika kuboresha miundombinu ya barabara kwa Kata zote 29 ambazo zitakuwa na changamoto ya barabara.

Kuhusu TASAF ,amesema Kata yake walengwa wapo na wanaendelea kunufaika na hizi siku mbili tatu walengwa watapatiwa fedha kwani Ofisi ya Mtendaji inaratibu vizuri zoezi la kuhakikisha walengwa wanapewa fedha.

Akizungumzia Vikundi vya Mkopo, Mhe. Mbilinyi amesema mikopo haijafutwa bali Serikali imesitisha kwa muda ili kuangalia namna bora ya kuboresha mikopo hiyo ya asilimia 10 inayotoka Halmashauri.

Katika hatua nyengine, ameitaka Jamii  kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali, wadau na asasi za kiraia katika kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na mabinti ili kujenga jamii yenye usawa.

Aidha, Mbilinyi, amesema Serikali imeweka sera na mikakati ya kupinga vitendo vyote vya ukatili na nguvu zaidi ni kwa jamii kushiriki kwa ukaribu katika kukemea na kuripoti vitendo hivyo.

Mhe. Mbilinyi, amewataka  Wananchi kujitokeza  kwa wingi Tarehe 26/11/2023 kwenye eneo la ujenzi wa Kituo cha Polisi Lukobe ambapo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Sanga ,atazungumza na wananchi  kuhusu ulinzi na usalama.

Kwa upande wa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro OCD ,Dennis Majumba amesema kuwa Kata ya Lukobe na Kata zote 29 wataendelea kuhakikisha usalama na ulinzi unaimarika.

OCD Majumba, amesema suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila mtu hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kulinda amani na usalama.

"Jukumu hili la ulinzi sio la Jeshi la Polisi, hata hawa mnaowaita ulinzi shirikishi wao wapo kuhakikisha usalama wa raia lakini sio kwamba ni jukumu lao moja kwa moja , dhana ya Polisi Jamii ni kuendelea kutoa elimu ili kupunguza uhalifu na wahalifu" Amesema OCD Majumba.

Kwa upande wa mratibu wa CHF Manispaa ya Morogoro, Saada Mkuya, amewataka wananchi kujiunga na mfuko huo wa afya ili kupunguza gharama  za matibabu wanapopata ugonjwa.

"Ugonjwa hauna hodi, niwaombe wananchi CHF ni bima nzuri sana iliyoboreshwa  fika Ofisi ya Kata utapata utaratibu gharama yake ni Shilingi 30,000/= kwa mwaka kwa  watu 6 kwenye Kaya moja" Amesema Mkuya.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.