TANGA JIJI YAFURAHISHWA NA MANISPAA YA MOROGORO UENDESHWAJI NA UKUSANYAJI WA MAPATO STENDI YA MABASI MSAMVU
HALMASHAURI ya Jiji la Tanga , imeipongeza Manispaa ya Morogoro kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ikiwamo mradi wa Stendi ya Mabasi Msamvu.
Akizungumza wakati wa ziara , Novemba 13/2023 , Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga,Mhe. Abdurahman Shiloow ambaye ndiye kiongozi wa msafara, amesema wamefurahishwa na namna ya uendeshaji wa Stendi hiyo , hivyo amelitaka Baraza la Madiwani Tanga Jiji kuhakikisha wanapo rudi nyumbani waanze kufanyia kazi kwa kile walichojifunza.
Amesema kuwa, Manispaa ya Morogoro inahitaji kupongezwa sana kwani wamepiga hatua kubwa huku wakionesha mtiririko mzuri wa makusanyo, na utaratibu wa mifumo wanayoitumia katika kudhibiti mapato yasipotee jambo ambalo wao imekuwa funzo na watajipanga kuhakikisha wanalifanyia kazi katika Stendi yao ya Kange.
Mhe, Shiloow, amefurahishwa zaidi jinsi Manispaa hiyo ilivyoweka vipaumbele hususani katika kuwapanga wafanyabiashara kwa maridhiano na kuwapa kipaumbele kufanya biashara hususani wajasiriamali kwenye Stendi ya Msamvu. .
"'Niwapongeze viongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani na Wataalamu, kazi inaonekana , kwakweli katika mradi huu wa Stendi kuna vitu vingi tumejifunza, sisi kwetu tuna miradi mingi lakini tumejifunza jinsi ya kuendesha mradi wa Stendi na tukirudi tutakwenda kukaa na wamiliki wa magari makubwa na madogo kuona jinsi gani tutazungumza kwa maridhiano ili na sisi tuanze kukusanya mapato , mapato yetu kwa mwaka ni Bilioni 19 ,sasa tukichukua na mapato ya stendi tutapiga hatua kubwa sana, kingine katika mradi wa stendi ya Msamvu tumeona wakaguzi wa kimataifa wanavyofanya kazi yao kwakweli inaonesha ni jinsi gani Manispaa yenu mlivyo karibu na Serikali pamoja na Chama Tawala CCM" Amesema Mhe. Shiloow.
"Ukiangalia Jiji letu la Tanga, tunataka kuibua miradi mikubwa lakini tunahitaji kukusanya kodi katika miradi hiyo, hivyo lengo letu kubwa kuja hapa ni kuona namna gani tutapata uzoefu na kujua wenzetu wanatumia aina gani ya ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi ili nasisi tuweze kufanya kama wanavyofanya wao japo sisi mapato yetu makubwa lakini kujifunza hakuna mwisho hata mtoto anaweza kujifunza kwa mkubwa " Ameongeza Mhe.Shiloow.
Hata hivyo, Mhe.Shiloow, amesema watamshauri Mkurugenzi wa Jiji pamoja na Baraza la Madiwani kuhakikisha mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa kupata utaratibu mzuri wa uendeshaji wa Stendi yao , waweke uongozi mzuri ambao wataamua katika Baraza lao na utakaokuwa unauwezo wa kukusanya fedha katika Stendi hiyo ili Jiji hilo liweze kuendesha miradi mingine "Amesema Mhe......
Naye, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe.Rehema Kasim Muhina, amesema siku zote katika kuhitaji maendeleo lazima ujifunze kwa mwenzako maana rasilimali pesa inakuwa ndogo kuliko idadi ya watu, hivyo wamejifunza jinsi ya kuendesha mradi huo vizuri, isije tena ikwawa wameibua mradi huo ,harafu mradi huo ukaleta migogoro na kutokuwa na tija kitu ambacho hakitawasaidia katika kufikia malengo yao ya kukusanya kodi.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, , ameipongeza Tanga Jiji kwa kujitolea kuja kujifunza namna ya kuendesha mradi huo wa kimkakati wa Stendi ya Mabasi Msamvu na jinsi ukusanyaji wa mapato.
Mhe. Kihanga, amesema kujifunza sio dhambi hivyo wataendeleza ushirikiano huo pindi pale watakavyohitajika kufanya hivyo kwa Ustawi wa Maendeleo ya Tanzania na Wananchi kwa Ujumla.
Aidha, Kihanga, amesema kuwa kujifunza ni njia ya kupata maendeleo zaidi ,hivyo kwa kupitia mafunzo hayo Jiji la Tanga watanufaika sana na wataimarisha mifumo ya kodi na kuiletea Jiji lao Mendeleo.
" Kweli tumewapokea ndugu zetu wa Tanga Jiji, kwa ajili ya kuja kujifunza hapa kwetu, matumaini yangu ni kwamba tangia walivyokuja ni tofauti na sasa baada ya kuondoka, lakini tunachowaambia mafanikio yetu ni kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za mradi, hivyo tunakusanya fedha nyingi lakini hizi fedha tunazipeleka kwenye miradi ya wananchi na miradi hiyo inaonekana, lakini Manispaa ya Morogoro tumekuwa na miradi mikubwa matarajio yetu baada ya miradi hii kukamilika tutakusanya pesa na tutazielekeza katika kuibua miradi mengine ya maendeleo"Ameongeza Kihanga.
Post a Comment