Header Ads

DIWANI TUNDA AOMBA USHIRKIANO KWA WANANCHI KUTIMIZA MIPANGO YA KUIVUSHA KATA YA KINGO


DIWANI wa Kata ya Kingo Manispaa ya Morogoro , Mhe. Amini Tunda, amewataka wananchi kutoa ushirikiano na Ofisi yake ili aweze kutekeleza vyema mikakati ambayo itaivusha Kata hiyo kusonga mbele.

Kauli hiyo ameizungumza Novemba 10/2023 katika Kikao cha wananchi cha kueleza utekelezaji wa Ilani  ya CCM tangia aingie madarakani kwenye eneo la Uwanja wa DDC Mbaraka Mwinshe nje ya Ukumbi huo wa Manispaa.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Mkutano huo, Mhe. Tunda, amesema umoja na mshikamano ndio utawavusha na kufanya utekelezaji wa kutimiza mahitaji ya wana Kingo.

"Tusipokuwa na umoja haya ambayo tunataka kuyafanya hayatafanyika, niombe muendelee na umoja wenu, muheshimu Serikali na chama chake kiliniweka madarakani ili  niweze kutimiza wajibu wangu wa kutekeleza vyema Ilani ya CCM " Amesema Mhe. Tunda.

Kuhusu sekta ya elimu, Mhe. Tunda amesema tangia aingie madarakani, amesimamia ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya Sekondari Kingo yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi kwa gharama ya Milioni 10 na Manispaa kukamilisha madarasa hayo kwa jumla ya fedha milioni 33 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021.

Aidha,amesema katika kipindi chake cha miaka 3 , amesimamia ukamilishaji wa Maabara moja ya kisasa Shule ya Sekondari Kingo iliyogharimu Milioni 29,519,000/= fedha kutoka Serikali Kuu.

Amesema kulikuwa na ujenzi wa madarasa 2 Shule ya Sekondari Kingo mwaka 2023  , madarasa ya mradi wa UVIKO-19 yaliyogharimu Milioni 40.

Mbali na ujenzi wa Madarasa lakini katika kipindi cha miaka 3 , amejenga matundu 10 ya Vyoo shule ya Msingi Mwere yenye tahamani ya Shilingi Milioni 10 fedha kutoka Manispaa ambapo mradi umefikia hatua nzuri ya kukamilika.

Kuhusu huduma ya maji, amejitolea upatikanaji wa kisima Shule ya Sekondari Kingo na sasa hakuna changamoto ya maji katika shule hiyo.

Mipango ya baadae, miongoni mwa mipango ambayo Mhe. Tunda, anatarajia kuifanya kwa kushirikiana na Uongozi wake wa Kata ni kuendelea kusimamia mpango wa Serikali wa elimu bila malipo, kuahasisha uundwaji wa Vikundi vya wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu, kusimamia upatikanaji wa chakula shuleni, kuendelea kuongeza madarasa, matundu ya vyoo kwa shule zote, kuendelea kuweka makambi kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha Nne Shule ya Sekondari Kingo, kufuatilia kudhibiti matukio ya ukatili wa kijinsia, kusimamia utunzaji wa mazingira, kuendelea kuhamasisha suala la ulinzi na usalama ikiwemo kusimamia uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi kwenye Mitaa pamoja na kufuatilia michango na kusimamia ujenzi wa Ofisi ya Kata kupitia nguvu ya wananchi.

Mwisho, Mhe. Tunda, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiletea fedha nyingi Manispaa ya Morogoro katika kufanikisha miradi ya maendeleo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.