Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro akabidhi TV na Kingámuzi vyenye thamani ya Shilingi 670,000/= Kituo cha kulelea Wazee wasijiweza Funga Funga.
Mwenyekiti wa Wazee kituo cha Funga Funga , Mzee Joseph Kaniki, akitoa salamu za pongezi kwa Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuwakabidhi zawadi ya TV. |
Wazee wakimsikiliza Mkurugenzi. |
Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro amekabidhi TV Flat Screen pamoja na Kingámuzi cha Star times kwa Wazee wasiojiweza katika kituo cha Funga Funga kilichopo Manispaa ya Morogoro.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya Shilingi laki 670,000/=, amevitoa ikiwa ni maombi ya Wazee hao.
Amesema lengo la kutoa Tv hiyo ni kuwafanya Wazee hao waweze kuangalia na kupata taarifa mbalimbali zinazoendelea na kuona maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
"Wazee wangu nimetoa hiki kidogo mlichokiomba, natumaini mnazo changamoto nyingi lakini tutaendelea kushirikiana Serikali na wadau wengine kuhakikisha hizo huduma nyengine zinapatikana kidogo kidogo kadri tunavyoweza kufanya lakini kikubwa Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt John Magufuli anawapenda sana mzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu afya njema na kuweza kutimiza majukumu yake ya kulifikisha Taifa hili kwenye Uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda"Amesema Sheilla
Amesema kuwa Mhe Rais . Dkt John Magufuli katika kipindi chake cha miaka 4 amefanya mengi sana yenye mafanikio ikiwamo miradi mikubwa ya kimkakati yenye kulenga ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) katika Mto Rufiji ambao mkandarasi ameanza rasmi utekelezaji wake, ununuzi wa ndege mradi wa Treni ya Mwendokasi ya Umeme (Standard Gauge Railway SGR).
Katika hatua nyengine, amewaeleza Wazee hao kwamba Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Manispaa zinazotekeleza miradi ya Kimkakati ikiwamo Stendi ya Mabasi Msamvu, Stendi Mpya ya Daladala iliyopo Mafiga pamoja na Ujenzi wa Soko kuu la Kisasa.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi Kituo cha Funga Funga, Bi Yolanda Komba,amemshukuru Mkurugenzi kwa msaada alioutoa hao kwani ilikuwa ni changamoto na kilio cha muda mrefu kwa Wazee hao.
Amemuomba kuendelea na moyo wa kuwasaidia kwani mbali na alichokitoa bado Wazee hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za huduma huku akimtakia kazi njema katika kutekeleza majukumu yake na kuanza mwaka mpya kwa mafanikio zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Wazee hao, Mzee Joseph Kaniki, ameushukuru Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kutekeleza kile walichokiomba huku akizidi kumuombea Mhe. Rais Magufuli afya njema ili aweze kuiongoza vyema Tanzana katika kufikia maendeleo hususani uchumi wa Kati na Viwanda.
Post a Comment