DC Moro awaagiza TARURA kushughulikia mitaro barabara ya Barakuda inayo tiririsha maji kwa Wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo akipitia ramani ya mipango miji , (kulia), Mbunge wa Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood. |
Mbunge wa Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood, akiwasalimia Wananchi katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero, (kulia), Mstahiki Meya Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga. |
Mstahiki Meya Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga akisaini kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika Kiwanja cha Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege leo. |
Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, (kulia), akimpokea Mkuu wa Wilaya, Mhe. Regina Chonjo mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege. |
Waheshimiwa Madiwani wa Kata kumi zilizoshiriki katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero wakiteta jambo. |
Mwananchi. |
Mwananchi akitoa kero. |
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, ameiagiza TARURA kufanya matengenezo ya haraka ya mifereji na mitaro iliyopo barabara ya Barakuda inayotiririsha maji kwa Wananchi.
Hayo ameyasema leo Januari 15,2020 kufuatia kero za wakazi wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo ,wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Chonjo, amemtaka Meneja wa TARURA kuhakikisha mitaro yote katika barabara hiyo inapanuliwa na kuyaelekeza maji yaende na sio kwa Wananchi.
Amesema kuwa miradi mikubwa kama hiyo ambayo Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, ameileta kwa ajili ya maendeleo ya wananchi isigeuke kero na kuleta maafaa badala ya kuifurahia.
"Nawaagiza TARURA hakikisheni hiyo michoro yenu mipya ya mitaro iende kwa aharaka na muitengenezee njia nzuri hii mitaro na kuyaelekeza maji kutiririka kabla ya mvua za vuli kunyesha na kusababisha maafa, na kama mtaona mnakwama wasiliana na Mbunge wa Jimbo la Morogoro, Mhe. Abdulaziz Abood, ili akaongee na Meneja wenu Taifa na kumfikishia Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi ili kero hiyo isilete maafa kwa wananchi wetu" Amesema DC Chonjo.
Akijibu kero hiyo, Meneja wa TARURA Manispaa ya Morogoro, Mhandisi James Mnene, amesema anafahamu changamoto hiyo lakini katika bajeti zao suala la matengenezo ya mitaro hiyo halipo mpaka pale watakapo kamilisha dizaini ya michoro mipya.
Amesema kuwa hadi kufikia ijumaa ya tarehe 16 Januari 2020, makabrasha yote yanayohusu taarifa za michoro yatakuwa yameshawasilishwa kwa Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro ili taarifa hizo ziweze kupatiwa Bajeti.
Aidha, amesema baada taarifa hizo kufika kwa Meneja wa TARURA Mkoa, pia wataziwasilisha katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
Katika hatua nyengine, DC Chonjo, amemtaka mkazi aliyebomolewa nyumba yake kupisha ujenzi wa Tawi la Benki ya NMB Wami, kulipwa stahiki zake zote anazodai.
Amesema kuwa miaka kadhaa iliyopita tangia kujengwa kwa Benki hiyo kwamba maeneo yote yalifanyiwa tathmini na wahusika walishalipwa pesa zao iweje huyo mpaka leo hajapewa haki zake.
Amesema haki ya mtu haipotei huku akiahidi kulifuatilia suala hilo na kuangalia taarifa za malipo katika Benki hiyo na kama itagundulika malipo yamefanyika na wahuni wamekula pesa hizo kesi hiyo itaanza upya na waliohusika watachukuliwa hatua kazi za kisheria.
"Hili suala tunalifuatilia maana kama Halmshauri itamps mtu huyo kiwanja mbadala wakati haki yake alitakiwa aipate nje ya hapo sio sahihi kwani ni bora eneo hilo litumike kwa ajili ya huduma kama vile Shule au kujenga Choo, tunakwenda Benki ili kujua ukweli wa jambo hilo na kumsaidia mwananchi huyu aweze kupata haki zake" Ameongeza DC Chonjo.
Akijibu juu ya maelezo aliyoyatoa Mkuu wa Wilaya, Afisa Ardhi wa Manispaa ya Morogoro, Msemwa Gizbert, amesema mchakato wa kugawa Viwanja mbadala upo na wanasubiri maamuzi yatakayotolewa kama mwananchi huyo apatiwe au la.
Aidha ameenda mbali baada ya kuwataka wavamizi waliovamia maeneo ya Mkonge ambayo hati zote zilifutwa na aliyekuwa Mhe. Rais wa awamu ya Tatu, mhe. Benjamini Mkapa watoke mara moja kabla ya kuchukuliwa hatua.
Pia amesema kumezuka tabia baadhi ya wakazi wa Kata ya Lukobe Kambi tano kujimilikisha ardhi waliyopewa kwa ajili ya kilimo lakini cha kushangaza maeneo hayo yamegeuzwa makazi ya watu jambo ambalo sio sahihi kisheria.
Amesema maeneo hayo mwaka 2006 yalipimwa lakini kinachoendelea ni kwamba watu wamefikia hatua ya kuyamega vipande vipande na kuyauza huku akisema kwa mujibu wa sheria za Mipango Miji maeneo hayo siyo ya Makazi ni kwa ajili ya huduma za Jamii.
Post a Comment