TARURA MANISPAA MORO YAWATOA HOFU MADIWANI KUHUSU MATENGENEZO YA BARABARA
Posted On: October 31st, 2019
Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Manispaa ya Morogoro kwa mwaka wa fedha 2019/2020 umeidhinishiwa kiasi cha Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi miwili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe.
Meneja wa TARURA, Manispaa ya Morogoro Mhandisi, Mnene James alisema hayo kwenye Kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani la Manispaa kilichofanyika Oktoba 31, 2019 kwenye ukumbi wa Manispaa.
Hata hivyo TARURA Manispaa ya Morogoro katika mwaka huu wa fedha iliwasilisha maombi ya miradi mitano iliyokuwa imeombea fedha kiasi cha Sh bilioni 1.9 .
Mhandisi James alisema hayo wakati wa kujibu swali la msingi la Diwani wa Kata ya Kihonda , Hamis Kilongo pamoja na hoja iliyotolewa na Diwani Zamoyoni Abdallah wa Kata Bigwa.
Madiwani hao kwa nyakati tofauti walimuuliza mstahiki Meya wa Manispaa , Pascal Kihanga kuhusiana na changamoto za ubovu wa barabara nyingi za Manispaa licha ya uwepo wa TARURA .
Kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Manispaa ya Morogoro kuwa , Manispaa ina jumla ya barabara zenye urefu wa zaidi ya kilometa 517 ambapo kwa nyakati hizi zipo kwenye hali mbaya.
Hata hivyo alisema , TARURA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha barabara hizo na kwa mwaka huu wa fedha ( 2019-2020) imeingia mikataba ya miradi miwili ya ujenzi wa barabara yenye kugharimu Sh bilioni 1.6.
Alisema , TARURA Manispaa ya Morogoro iliwasilisha miradi mitano na kuombea fedha kiasi cha Sh bilioni 1.9 , lakini ilipofika kipindi cha manunuzi yalitolewa maelekezo ya kupunguza asilimia 20 ya bajeti iliyoombwa ya miradi mitano na kubakiwa na miradi miwili yenye kugharimu Sh bilioni 1.6.
Mhandisi wa TARURA Manispaa ya Morogoro alitaja baadhi ya barabara zilizopo katika mradi wa kwanza ni kata ya Boma , Mji Mkuu, Mbuyuni , Lugara – Lukobe , wakati mradi wa pili utahusisha kata ya Kihonda Magorofani, Kihonda- Mkundi, Mafisa na Mazimbu.
“ TARURA Manispaa ya Morogoro tayari imeziandikia kata husika barua ikizijulisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara wa kiwango cha changarawe “ alisema .
Pamoja na hayo alisema , TARURA itaendelea kutengeneza barabara za Manispaa kila itapopata fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa barabara .
Post a Comment