DC Mjema atoa agizo TAKUKURU kuingilia kati Mgogoro wa Ukuta ulioziba bara bara Mtaa wa Ugombolwa Kata ya Segerea .
MKUU wa Wilaya Ilala Mh Sophia Mjema , ameiagiza TAKUKURU kufuatilia mgogoro uliopo katika Mtaa wa Ugombolwa Kata ya Segerea juu ya malalamiko ya wakazi hao kuuzibiwa bara bara kutokana na mkazi mmoja kujenga ukuta .
Agizo hilo amelitoa leo Oktoba 16 mwaka 2019, akitembelea eneo hilo katika ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi ikiwa ni kata ya 22 miongoni mwa kata 36 zilizopo Wilaya ya Ilala.
Amesema hata kama mlalamikiwa ana hati ya nyumba, lakini bado Manispaa ina wajibu wa kutengua hati hiyo kwa ajili ya manufaa ya watu wengine.
" TAKUKURU nawakabidhi kazi hii, haiwezekani kila mara tunatoa maagizo hayafanyiwi kazi, sasa kama kuna vimelea vya rushwa wale waliohusika kamata tia ndani" Amesema Mjema.
Amewataka maafisa Ardhi na watu wa mipango miji kuhakikisha wanapofanya urasimishaji wa Viwanja na maeneo waangalie suala la bara bara wakati wanatoa hati za Viwanja.
Kwa upande wa Mlalamikaji wa Wananchi waliozibiwa bara bara, Ndugu Hussain Mmali, amesema mlalamikiwa, Ndugu Kileo , amekua mkaidi sana katika kufikia suluhu juu ya kuziba bara bara.
Amesema ni zaidi ya vikao 11 wamekaa pamoja na Mtendaji wa Kata na Viongozi wa Mitaa lakini hajawahi kutokea wala kutoa taarifa.
" Tunateseka sana Mh DC, kila tukichukua hatua lakini hakuna maamuzi yanayofanyika, ametufanya tuwe tunapita vichochoroni, hata ukiangalia ule uchochoro tuliopita ni kanisa wamefanya huruma ya kutumegea eneo lao ndani ya kanisa, hata maelezo yake alisema uchochoro uliobakia watapita watu lakini cha kushangaza ameanza ujenzi kwa lengo la kuziba eneo lote sisi tutapita wapi Mkuu? Kulitokea nyumba kuungua moto lakini Zima moto hawakuweza kufika kutokana hakuna bara bara" Ameeleza Ndugu Mmali kwa masikitiko makubwa.
Post a Comment