Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAKUTANA NA WADAU KUJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI

Posted On: October 30th, 2019
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi kwa lengo la kujadili taarifa iliyoandaliwa na mtaalamu mwezeshaji kutoka shirika la FOSEWERD Initiative Limited ya Jijini Dodoma kwa kushirikiana na wataalamu wa manispaa h iliyoainisha fursa za uwekezaji zilizopo katika Manispaa ya Morogoro.
Akifungua kikao hicho cha majadiliano Meya wa Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga alisema kuwa katika taarifa hiyo imetajwa mikakati ya kuvutia wawekezaji, jinsi gani ya kuzinadi fursa za uwekezaji, changamoto za uwekezaji na pia imetoa mapendekezo ya namna gani ya kutatua changamoto ili kuchochea ukuaji wa biashara na uwekezaji katika manispaa.
Meya Kihanga alisema kuwa Serikali inawajibu wa kushirikiana na sekta binafsi kufanikisha azma ya kujenga uchumi imara wa Halmashauri, mkoa na nchi kwa ujumla.
Aidha Kihanga alisema kuwa Serikali inawajibu mkubwa wa kuhakikisha inaboresha mazingira rafiki na wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba miundombinu ikiwemo ya mawasiliano, usafirishaji na nishati inakuwa bora.
Pia Serikali inawajibu wa kufanya marekebisho ya kanuni ama sheria ndogo zinazotajwa kuwa ni vikwazo kwa uwekezaji au uendeshaji biashara na kutoa mrejesho wa marekebisho ya kanuni na sheria hizo kwa wawekezaji.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chemba ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima TTCIA Mwadhin Myanza alisema kuwa taarifa hiyo ya fusra za uwekezaji itasaidia kuweka mikakati mizuri ya uwekezaji kwa kuwa imetaja maeneo ya uwekezaji, aina za uwekezaji na namna ya kukabiliana na changamoto za uwekezaji.
Hata hivyo Myanza alisema kuwa TCCIA imeweka kipaumbele katika kuhimiza utoaji wa huduma za pamoja (One stop center) ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabishara ambao wamekuwa wakisumbuka kupata huduma za kibiashara zikiwemo za TRA.
Naye meneja masoko wa kiwanda cha kubangua mpunga cha MW cha Morogoro Matha David alisema kuwa midahalo na majadiliano yanayohusu uwekezaji yamekuwa yakisaidia kupunguza changamoto mbalimbali zinazokwaza kwenye uwekezaji.
Kuhusu Changamoto Matha alisema awali umeme ulikuwa ukikatikakatika lakini kwa sasa tangu wameanza uzalishaji tatizo hilo limekwisha na pale inapotokea hitirafu Tanesco wamekuwa wakitoa taarifa kabla hawajakata umeme hata hivyo alitaja changamoto ya maji kuwa bado inakwaza wawekezaji wengi hasa wale ambao bidhaa wanazozalisha zinatumia maji.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.