DC Mjema agiza Kampuni ya Kajenjere kusimamishwa kazi ya uzoaji taka taka Kata ya Mnyamani.
.
MKUU wa Wilaya Ilala Mh Sophia Mjema amesimamisha tenda ya usafi kampuni ya Kajenjere Ltd kufuatia malalamiki ya Wananchi kuhusu bei ya tozo ya taka taka. .
Akizungumza na Waandishi wa Habari, amesema kampuni hiyo imekuwa ikilalamimiwa sana katika tozo za usafi hivyo ameitaka isimamishe kazi yao na kuwapa fursa Wananchi kutafuta kampuni watakayoweza kupanga nao tozo ambayo Wananchi wana uwezo nayo.
Amesema kuwa, tenda ya Kampuni ya usafi lazima iidhinishwe kupitia vikao vya Wananchi kwa makubaliano ya tozo watakazo panga wao kulingana na uwezo wao.
" Nafikiri kampuni hii ilipewa tenda hii kupitia manispaa yetu baada ya kukidhi vigezo, iweje Leo kila kona malalamiko ni hayo hayo tu, sasa niwaombe Wananchi mkae vikao na watu wa usafishaji wa Manispaa pamoja na viongozi wenu ili muweze kutafuta kampuni nyingine mtakayoweza kukubaliana nao tozo mtakazoona mna uwezo nazo " Amesema DC Mjema.
Kwa upande wa Meya wa Manispaa ya Ilala na Diwani wa Kata ya Vingunguti, Mh Omary Kumbilamoto, amepiga marufuku Mkuu wa Idara ya Mazingira kukaimisha mtu badala yake ahudhurie katika ziara ili aweze kujionea hali halisi ya changamoto katika Idara yake.
" Leo iwe mwisho na mwanzo , Mkuu wa Idara ya Mazingira kukaimisha mtu, nataka aje mwenyewe, nitajitahidi kutenga muda wangu hizi ziara zilizobakia nihudhirie nimuone jinsi anavyoweza kujibu kwa kina kero za Mazingira kwa Wananchi " Amesema Meya Kumbilamoto.
Amesema Idara ya Mazingira imekuwa ikiwaangusha katika kushughurikia kero za usafi na kuacha Wananchi wakizidi kuilalamikia Serikali kwa uzembe wao wa kutokuwa wafuatiliaji. Naye mkazi wa Mnyamani, Kuruthumu Omary, amempongeza Mkuu wa Wilaya Mh Sophia Mjema kwa utenguzi wa tenda kwa kampuni ya Kajenjere Ltd huku wakitaka ushirikishwaji zaidi wakati wa kutafuta kampuni mpya watakayoingia nayo mkataba wa usafisha na uzoaji taka kwa bei watakayo weza kukabiliana katika malipo.
Katika hatua nyingine, Afisa TAKUKURU Mkoa wa Ilala, Ndugu Damas Parsalaw, amemtaka bibi Afya kata ya Mnyamani pamoja na Afisa Mazingira kupeleka mkataba wa tenda ya usafi dhidi ya Kampuni ya Kajenjere katika kata hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa kina na kusisitiza kama wakigundua kuna vimelea vya upigaji au rushwa wahusika wote watachukuliwa hatua.
Pia amesema kama kuna pesa zilichukuliwa kwa Mwananchi kienyeji zirudishwe haraka huku akimtaka Meya wa Manispaa kuwa mkali na watendaji wake katika utendaji wa kazi ili kuhakikisha miradi yote iwe inawanufaisha Wananchi kwa malengo yaliyokusudiwa.
Post a Comment