DC Mjema aisimamisha kazi Kampuni ya Dimwe Survey Consultant kufuatia malalamiko ya ukusanyaji na utozaji fedha za urasimishaji na upimaji wa Ardhi.
MKUU wa Wilaya Ilala Mh Sophia Mjema, ameisimamisha kazi Kampuni ya urasimishaji na upimaji wa ardhi , Dimwe Survey Consultant, kufuatia malalamiko ya Wananchi wa Viwege ya kutoridhishwa na makusanyo na tozo za fedha za urasimishaji na upimaji wa Ardhi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, amesema Kampuni hiyo imekuwa ikilalamikiwa kutotoa risiti kupitia EFD Mshine badala yake risiti wamekuwa wakitoa kwa maandishi.
Amesema kutotoa pesa kwa mfumo wa EFD mashine ni kosa kubwa kwani linainyima Taifa pato na kuchelewesha Maendeleo.
" Hili halikubaliki, Serikali hii chini ya Rais Dkt John Magufuli imedhamiria kukusanya kodi kwa Maendeleo ya Taifa, sasa Afisa Ardhi naisimamisha kazi Kampuni hii kuanzia leo isijihusishe na kazi hiyo mpaka wajulishe jinsi wanavyokusanya na kutoza fedha za urasimishaji na upimaji" Amesema Mjema.
Naye Afisa Ardhi Manispaa ya Ilala, Ndugu Burton Rutta, amesema Kampuni hiyo imekuwa katika lawama na Wananchi kutokana na kutorejesha taarifa za urasimishaji na upimaji kwa Wananchi.
" Lazima ieleweke kwamba, zoezi la urasimishaji na upimaji linakiwa ushirikiano baini ya Serikali za Mtaa na Wananchi, lakini wao hawafanyi hivyo, kwa hali hii ndio maana migogoro ya ardhi haimaliziki kutokana na uzembe kama huu" Amesema Burton.
Aidha, amesema kutokutoa taarifa za urasimishaji na upimaji linachangia kwa kiasi kikubwa kuleta migogoro ya ardhi.
Amesema baada ya ziara kukamilika Ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya mipango miji ,watakaa kwa ajili ya kuyapitia malalamiko hayo na wakijiridhisha kuwepo kwa malalamiko hayo wataichukulia hatua Kali za kisheria Kampuni hiyo ikiwemo kurudisha pesa na kuinyang'anya tenda.
Post a Comment