Header Ads

​WAVUVI WATAKIWA KUPIGA VITA UVUVI HARAMU



WAZIRI  wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.  Abdalah Ulega, amewataka wavuvi kupinga vitendo vya uvuvi haramu na kutunza Rasilimali za Uvuvi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Waziri Ulega, ameyasema hayo alipokuwa akiongea na wavuvi wanaofanya shughuli zao Wilaya ya Kilombero waliopo  Halamshauri ya Mji Ifakara na Halamshauri ya Wilaya ya Mlimba Julai 05/2023.

Aidha, Mhe. Ulega, amesema kuwa uvuvi haramu ni sumu kwa biashara ya Samaki na Dagaa hivyo ni muhimu kuendelea kuutokomeza ili rasilimali za uvuvi ziweze kuwa na tija kwa Taifa.

"Anayefanya uvuvi haramu hatutakii mema sisi na watoto wetu, kwa hiyo huyo ni adui namba moja kwetu sisi sote,niombe tuzingatie sheria ili kuepusha migogoro na Serikali ,lazima tuwe na vibali vya uvuvi ,kwani uvuvi harama madhara yake ni makubwa  kama vile kusababisha kansa kwa walaji wa samaki " Amesema Mhe. Ulega.

Mhe. Ulega,  pamoja na kuwapongeza wavuvi hao kwa jitihada wanazozichukua katika kupinga vitendo vya watu wachache wanaofanya uvuvi haramu,amewahimiza wavuvi  kuendelea kupinga vitendo hivyo ili rasilimali hizo ziweze kuleta manufaa kwa Taifa na kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Kilombero.

Katika hatua nyengine, Waziri Ulega, amewataka wafugaji wabadilike kwa kumiliki ardhi zao kwa ajili ya mifugo yao.

" Wafugaji mbadilike, milikini ardhi zenu kwa ajili ya mifugo badala ya kua na mifugo mingi isiyo na mahala pa kuitunzia hali inayosababisha migogoro kati ya wafugaji na wakulima" Ameongeza Waziri Uledi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro. Mhe. Adam Malima, amesema  pamoja na shughuli hizo za uvuvi kuendelea kuwapatia kipato wavuvi na Serikali, lengo la Serikali ni kuona rasilimali hizo zinavuliwa kwauendelevu ili ziweze kurithishwa kwa vizazi vijavyo.


RC Malima, amewataka wananchi wa Kilombero kuwa na imani na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwaomba wasiishi kwa mazoea kwa kuwa mifugo sio laana ni baraka.

" Wafugaji tusiwachukie wakulima na wakulima tusiwachukie wafugaji wote tunategemeana, kwa hiyo wakulima wakiwa na maeneo yao ya ufugaji migogoro hii itaisha kwa kuwa kila mtu atakuwa na eneo lake la utawala wa kazi zake, na ifike wakati sisi wananchi tujivunie kuwepo na wakulima na wafugaji" Amesema RC Malima.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dastan Kyobya, ameshukuru ziara ya Waziri na kuahidi kutekeleza maelekezo yote na kuhakikisha migogoro ya wakulima na wafugaji inapatiwa ufumbuzi ili kuiletea Maendeleo Wilaya hiyo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.