Header Ads

TASAF MANISPAA YA MOROGORO YAZINDUA MRADI WA KIVUKO CHA WATEMBEA KWA MIGUU MISUFINI CHAMWINO.


KITENGO cha TASAF Manispaa ya Morogoro kimezindua mradi wa Kivuko cha watembea kwa miguu Mtaa wa Misufini Kata ya Chamwino.

Kituo hicho kimezinduliwa Julai11/2023  na Diwani wa Kata ya Chamwino, Mh. Abdallah Meya akiongozana na Mratibu wa TASAF Manispaa ya Morogoro , Feliciana Katemana, Afisa Ufuatiliaji TASAF Manispaa ya Morogoro, Judith Woisso, pamoja na Viongozi wa Kata.

Akizungumza katika zunduzi huo,Mhe. Meya, amesema  moja ya changamoto kubwa iliyokuwa kero  kwa wananchi  na kuwapa usumbufu ni kivuko, kwani wamekuwa wakipata shida sana wanapotumia barabara wakati wanapoenda katika majukumu yao au kupata huduma za kijamii.

Meya, amewataka Viongozi wa Mtaa huo kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha kuwa mradi huo unadumu ili kuendelea kutumika zaidi na kutoa huduma ya usafiri.

"Kivuko hiki kimewaondolea adha wananchi sasa hivi watembea kwa miguu wanapita bila shida, isipokuwa gari, na wala hatutawavumilia ambao watakuwa na malengo ya kuharibu miundombinu hii, watakaohusika tutawachukulia hatua kali za kisheria" Amesema Mhe. Meya.

Kwa upande wa Afisa Ufuatiliaji TASAF Manispaa ya  Morogoro, Judith Woisso,amesema mradi huo umekuwa ukiwalenga zaidi wanufaika wa TASAF katika kuongeza kipato kwani wamekuwa sehemu ya ujira katika kipindi chote cha ujenzi wa mradi huo.

Naye Mratibu wa TASAF Manispaa ya Morogoro, Feliciana Katemana, amesema kuwa kivuko hicho kitasaidia sana Jamii kupita kwa urahisi kwani awali wananchi wamekuwa wakiteseka kuvuka hapo.

" Hiki kituo kimekuja wakati muafaka, wananchi wanaopita eneo hili walikuwa wanateseka sana, bodaboda hazipiti vizuri lakini hata wagonjwa wakizidiwa unakuta usafiri haufiki ni changamoto, niombe kivuko  hiki kitunzwe na ni kwa bodaboda na watembea  kwa miguu ndio uwezo wa kubeba vitu hivyo na sio magari makubwa " Amesema Katemana.

Katemana amesema, katika ujenzi huo, Manispaa ya Morogoro imechangia asilimia 25 ya vifaa vya ujenzi na asilimia 75 imetokana na nguvu kazi za wananchi wa Mtaa huo wa Misufini.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Misufini, Ndg. Names Mkiwa, ameushukuru Uongozi wa Manispaa chini ya Kitengo cha TASAF kwa kuwapa mradi huo ambao utakuwa mkombozi kwa watembea kwa miguu ambao walikuwa wakipata shida kuvuka eneo hili hususani kipindi cha Mvua.

Mmoja wa wanufaika wa TASAF Mtaa wa Misufini, Sabina Lumongolo, amesema awali wananchi walikuwa wakipata tabu hadi inafika wakati wanakwenda ngazi za juu kuona kero na kufikia hadi wagonjwa na wajawazito wanapata shida kwa kuwa wananchi wa Mtaa huo na wale wanaotokea maeneo mengine ili wapate huduma ya afya na huduma nyengine ni lazima wavuke mfereji huo wa maji .

"Tunaishukuru TASAF kutujengea kivuko, kabla ya kujengwa wananchi walihangaika sana ,mvua ikinyesha mfereji unajaa maji,inabidi msubiri maji yapungue ndipo mvuke, wakati wa mvua hata watoto kwenda shule ni shida ,tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za TASAF kutusaidia sisi kwani tunanufaika na mradi lakini hata mahitaji tulikuwa tunapata kupitia ujira wa mradi huo" Amesema Lumongolo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.