Malezi ya mzazi huandika hatima ya mtoto wake
Na Yusuph Mwamba
UCHAMBUZI: Malezi ya mzazi huandika hatima ya mtoto wake
· Ni kutokana na nafasi ya muda mwingi wa kuishi na mtoto tangu
anapozaliwa, hivyo anakuwa na sifa za kuwa mwandishi wa hatima ya mtoto husika.
Mzazi ana nafasi ya pekee katika kumwandalia mtoto hatima ya
maisha. Ni mtu anayemtunza, kumhudumia na kumfundisha mtoto mpaka akue. Anaweza
kumwambukiza tabia njema au mbaya.
Ni kutokana na nafasi ya muda mwingi wa kuishi na mtoto tangu anapozaliwa,
hivyo anakuwa na sifa za kuwa mwandishi wa hatima ya mtoto husika.
Kiuhalisia hakuna mzazi anayetamani mwanaye awe na tabia mbaya.
Kila mzazi ana shauku ya tabia nzuri kwa mwanaye. Anatamani mtoto wake
ajinasibu kwa kutenda matendo mema ambayo yatarudisha sifa kwake.
Malezi ya wazazi ndiyo msingi wa kutabiri maisha ya siku za mbele
ya mtoto kitabia. Kimazingira, haipingiki kwamba mzazi ndiye darasa msingi la
malezi ya watoto. Wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha hawakosei hata hatua
moja katika malezi.
Hakuna mzazi ambaye angependa hatima ya mwanaye iwe ya misukosuko
lakini ni vyema kuangalia malezi wanayowapa watoto.
Ikumbukwe kuwa mtoto anajifunza na kuiga yale yanayomzunguka tangu
akiwa mchanga. Kama mzazi atakosea kumfunda mtoto, ni dhahiri hata ujana wake
utakuwa ovyo.
Pengine lawama nyingi kwa kipindi hiki zinazowaandama watoto na
vijana ni matokeo ya malezi kutoka kwa wazazi. Vijana wengi wamekosa mwelekeo
wa kimaadili, heshima na kitabia. Wamegubikwa na tabia ambazo hazina ladha
katika jamii. Haya yanawezekana kuwa ni matokeo ya familia wanazotoka.
Mathalani, kama wazazi ndani ya familia hawaheshimiani, hawatoi
picha ya thamani ya kuheshimiwa, vivyo hivyo watoto nao watakuwa na ujasiri wa
kutoheshimu wakubwa. Tusitegemee miujiza ya kuwafanya.
Kwa nyakati hizi, siyo kitu cha kushangaa kuwakuta watoto
wanajibizana na wazazi tena kwa kukaripiana na wakati mwingine wazazi kwa kuona
aibu wananyog’onyea na kuwa wapole ili kumaliza mambo, kitu ambacho kwa mantiki
ya kawaida kinawapa watoto nguvu na kiburi cha ushindi.
Si kitendo kibaya mtoto kujibizana na mzazi kwa kuwa kinampa mtoto
mawanda mapana ya kuhoji kile ambacho hajaridhia kukitenda.
Tatizo ni pale linapokuja suala ambalo linahitaji nafasi ya mzazi
ijidhihirishe kwa mtoto, lakini kwa kuwa mtoto amepewa uhuru uliopitiliza na
mazoea yasiyokidhi viwango, anajiinua na kutaka kuififisha nafasi ya mzazi.
Mathalani, mtoto anapofanya makosa ni wajibu wa mzazi kumwelekeza,
kumkanya hata ikibidi kumpa adhabu. Viboko ni njia sahihi ya kumrudisha mtoto katika
nafasi nzuri kinidhamu. Hata kwenye vitabu vitakatifu vimeelekeza kuwa
usimnyime mwanao fimbo.
Wapo watoto ambao kwenye familia hata kama wakikosa hawashikiki
kwa kuwa wameona mazingira ya wazazi yanawaruhusu kukataa adhabu. Haya ni
matokeo ya malezi katika familia.
Athari kama hizi ndizo zinazowasukuma baadhi ya wanafunzi
kuwadharau walimu shuleni, hata pale wanapofanya makosa kukataa kuadhibiwa.
Wazee wetu wanatuambia zama zao ukifanya kosa shuleni ungetandikwa
viboko na mwalimu, ukirudi nyumbani mzazi naye anakuongezea adhabu.
Hali hii ilitokana na malezi ambayo wazee walikuwa wanawapa watoto
wao. Yalikuwa malezi ya kutambua nini maana ya mzazi lakini pia malezi
yalimfanya mtoto atambue ni nani anayeweza kumwadhibu pale anapokosea.
Tofauti na zama za sasa ambazo mazingira hayampi mzazi wa mwingine
kumuonya mtoto wa mwenzake, wala hayampi mwalimu mamlaka ya kujisikia amani
pale anapomwonya mwanafunzi.
Si muumini wa kushadadia viboko, lakini ninachomaanisha ni mzazi
au mwalimu kuwa na uhuru wa kumkanya mwanafunzi pale anapofanya makosa.
Kwa kiasi kikubwa maadili na malezi kwa watoto na vijana
yameporomoka, tunapoyafumbia macho yanazidi kuota mizizi na kuzidi kuandika
hatima mbaya kwa watoto.
Kwa mfano, kijana anaweza kukutana na mzee njiani na kijana asimsalimie.
Hili linajaribu kuleta tafsiri kuwa hayo ndiyo malezi na maisha ambayo kijana
anaishi na wazazi wake.
Kwa upande mwingine tunaweza kuwalaumu watoto na vijana ilhali
tukisahau kuwa wazazi ndiyo waandishi wa hatima za watoto wao.
Hii ina maana kwamba, namna wanavyowalea, wanavyowaonya na
wanavyoishi nao ndivyo wanavyowatengenezea mfumo wa maisha.
Wahenga walisema, “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Hivyo wazazi wanakumbushwa kuwa tabia nzuri ni matokeo ya msingi wa malezi ndani ya familia.
Post a Comment