WANAFUNZI 640 KUCHAGULIWA KWA UFADHILI WA SAMIA SCHOLARSHIP
WANAFUNZI wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi na
hisabati wana nafasi ya kupata ufadhili wa asilimia 100 kwa masomo ya elimu ya
juu kupitia mpango wa Samia Scholarship unaotarajiwa kuanza mwaka wa masomo
2023/24.
Mpango huo ulioanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka
2022 unalenga kuongeza idadi ya wanasayansi nchini ambao watachangia katika
maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa
wanafunzi 640 watachaguliwa kwa ufadhili huo kwa kuzingatia vigezo vya ufaulu,
tahasusi na programu za masomo.
“Samia Scholarship ni fursa kubwa kwa wanafunzi wetu wenye
vipaji katika sayansi na hisabati. Tunawasihi watumie fursa hii kujipatia elimu
bora na kujiandaa kuchangia katika ujenzi wa taifa letu,” amesema Prof. Mkenda.
Ufadhili huo
utagharamia ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, vitabu na viandikwa,
utafiti, bima ya afya, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo na vifaa
saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Maombi ya ufadhili huo yatawasilishwa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa
https://olas.heslb.go.tz kuanzia Jumatatu, Septemba 25, 2023 na orodha ya
majina ya wanafunzi wenye sifa za kuomba itapatikana kupitia www.moe.go.tz na
www.heslb.go.tz kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi Agosti, 2023.
Ameongezea kwa kusema kuwa wanufaika wa ufadhili huo
watapaswa kusoma, kuelewa na kusaini mkataba wa makubaliano ya ufadhili wa
masomo kati yao na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Wanufaika hao hawataruhusiwa kubadilisha programu za masomo
waliyopatiwa ufadhili bila idhini ya maandishi kutoka Wizara hiyo, na pia
hawataruhusiwa kuahirisha masomo isipokuwa kwa sababu za kiafya
zinazothibitishwa na chuo husika.
Prof. Mkenda ametoa wito kwa wanafunzi wenye sifa za kuomba
ufadhili huo kutumia fursa hiyo adhimu na kujiandaa vizuri kwa ajili ya masomo
yao.
“Samia Scholarship ni zawadi kutoka kwa Rais wetu mpendwa
Samia Suluhu Hassan. Tunamshukuru sana kwa moyo wake wa uzalendo na upendo.
Tunawaomba wanafunzi wetu wawe wazalendo pia na kutumia vizuri fursa hii,” amesema
Prof. Mkenda.
Post a Comment