MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA MASHUJAA
MANISPAA ya Morogoro imeadhimisha Siku ya kumbukizi ya Mashuja ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe.Adam Malima.
Maadhimisho hayo yamefanyika Julai 25/7/2023 kwenye mnara wa Mashujaa mkabala na Ofisi Kuu ya Manispaa.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo, RC Malima, amesema wanawakumbuka Mashujaa kwani walipambana kwa hali na mali kwa ajili ya kuitetea Nchi ya Tanzania wakiwa katika Maeneo mbalimbali kwani walijizatiti na kujitoa kwa uzalendo mkubwa kwa kuweka rehani Maisha yao kwa ajili ya Tanzania.
" Leo tunafanya kumbukizi ya Mashujaa wetu lakini mkumbuke kuwa Misingi mizuri na imara iliyojengwa wasisi wa Taifa letu baba wa Taifa ,Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere Na Sheikh Abeid Amani Karume,imesababisha Wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu kuishi kwa Amani na Utulivu,huku wakifanya mambo yao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote wa ndani au nje, amani iliyojengwa na imepelekea wageni,wakimbizi na watalii kuifanya Tanzania kuwa kivutio na kimbilio" Amesema RC Malima.
Aidha, amewataka wananchi kuithamini na kuilinda amani ya Tanzania kwa kuwa amani na utulivu uliopo haipatikanini katika mataifa mengine na mataifa mengi wanaitamani na kuitafuta bila mafanikio.
Hata hivyo, amewataka wananchi na Watanzania kwa ujumla, kuendelea kuienzi na kuilinda Amani iliyopo kwani amani ni sawa na yai mkononi ukilivunja hautaweza kulinganisha kamwe na pia amani haina bei na ikipotea haina soko la kununua.
Naye Chifu Kingalu, amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutambua Machifu waliopo na kushirikishwa kwenye masuala mbalimbali ya Kitaifa.
Chifu Kingalu, amewataka Watanzania kuliombea Taifa pamoja na Viongozi wake huku wakiendelea kuitunza na kuilinda amani iliyopo kwa Ustawi mpana wa nchi.
Maadhimisho ya Mashujaa yameambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo dua na sala maalum ya kuwaombea mashujaa waliopoteza maisha na kuiombea amani nchi kutoka kwa viongozi wa dini pamoja gwaride maalum kwa ajili ya mashujaa wetu.
Post a Comment