Header Ads

WEZESHA MABADILIKO YAGAWA PEDI 300 KWA WANAFUNZI WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU SEKONDARI MANISPAA YA MOROGORO




TAASISI ya Wezesha Mabadiliko (WEMA ) imegawa Pedi 300 kwa wanafunzi wanaoishi katika Mazingira magumu  kwa shule 10 za Sekondari Manispaa ya Morogoro katika Kongamano la Mtoto wa Kike kwa Shule za Sekondari lililoandaliwa na Taasisi hiyo.

Ugawaji huo wa pedi ulioendana na utoaji wa elimu ya kujitambua, hedhi salama na ukatili wa kijinsia ,umefanyika Julai 28/2023  katika Ukumbi wa Kingo Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.

Akizungumza katika  kongamano hilo la Mtoto wa Kike, Bi. Flora Yongolo, ameipongeza WEMA kwa kuwajali wasichana katika kujistiri na hedhi shuleni.

Yongolo, amesema pamoja na jitihada zinazofanyika kuhakikisha kuwa na vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi lakini bado changamoto kubwa ni upatikanaji wa vitambaa wakati wa hedhi "pedi"kwa watoto wa kike hasa kwa watoto wasio na uwezo.

Amesema  kuwa kumekuwa na changamoto za pedi kwa wanafunzi wa kike hususani wanaoishi katika mazingira magumu  kwani  bajeti inayotolewa na serikali katika Sekta ya Elimu  haijitoshelezi kuhudumia wanafunzi wote wa kike katika shule kwa kuwanunulia pedi.

Naye Mkurugenzi wa Wezesha Mabadiliko (WEMA) Dr. Lusako Mwakiluma, amesema wamekuwa na utaratibu wa kugawa pedi kila mwaka kwa watoto wa kike  kwani  shule nyingi hazina uwezo wa kifedha kuweza kununua pedi na kuzigawa bure kwa wanafunzi.

Dr. Lusako, amewaomba wadau  mbalimbali  kujitokeza kusaidia watoto wa kike kwani wazazi wengi wamekuwa wakidai hawana uwezo wa kununua vitambaa hivyo.

"Tumegawa pedi kwa watoto wetu, lakini tumeona wapatiwe na semina  elekezi ili kuwajengea uwezo watoto wa kike ili waweze kujitambua na kujua nafasi zao katika familia na jamii inayowazunguka" Amesema Dr. Mwakiluma.

Kwa upande wa Kaimu Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro, Herieth Kagosi, ameishukuru Taasisi ya Wezesha Mabadiliko kwa jitihada zao katika ustawi wa elimu Manispaa ya Morogoro.

" Wezesha Mabadiliko wamekuwa wadau wetu wakubwa sana, shule yetu ya Sekondari Uluguru wametujengea choo cha kujistili Mtoto wa kike, wametuwezesha kuwapa morali waalimu na wanafunzi matokeo ya kidato cha nne mwaka 2022 shule ya Uluguru haikuwa na zero ,hii imeonesha ni kwa jinsi gani wadau hawa walivyo na tija katika Manispaa yetu ya Morogoro" Amesema Kagosi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walimu waliombatana na wanafunzi kutoka shule 10 za Sekondari Manispaa ya Morogoro, wamesema  wamejitahidi kuwa na vyumba maalumu kwa ajili ya watoto wa kike kujistiri wanapokuwa kwenye hedhi lakini changamoto ni upatikanaji wa pad kwani watoto wengi hawana uwezo wa kununua pedi.

Upande wa Mwakilishi wa wanafunzi shule ya Sekondari 88, Sabrina Omary, amesema ukosefu wa pedi unafanya baadhi ya wanafunzi wa kike kutohudhuria masomo wanapokuwa katika siku zao ‘hedhi’, hivyo tunamshukuru Mkurugenzi Wezesha kwa kutusaidia hizi pedi ili tuendelee kujiimarisha tukiwa safi shuleni tunapofikia hali hii ya hedhi.

Shule ambazo ziliwapitiwa pedi ni Shule ya Sekondari 88, Mwembesongo, Uwanja wa Taifa, SUA, Mazimbu, Kihonda ,Mafiga, Uluguru, Kingo na Kayenzi.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.