Mkurugenzi Manispaa Morogoro atekeleza agizo la Waziri Mkuu ujenzi wa makaburi ya waliofariki kwa ajali ya Moto.
Muonekano wa Uzio wa Makaburi ya walifariki kwa ajali ya Moto Morogoro kufuatia mlipuko wa Lori la Mafuta. |
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akikagua eneo ambalo litatumika kujenga Mnara wa marehemu. |
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akitoka katika uzio wa makaburi mara baada ya ukaguzi kumalizika. |
MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,
amesema tayari Manispaa ya Morogoro imeshachukua hatua za haraka za kutekeleza agizo
la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Mjaliwa , la ujenzi
wa Makaburi pamoja na mnara kwa walifariki na ajali ya moto.
Kauli hiyo ameitoa leo Mei 14, 2020 ,mara baada ya
kuzuru katika makaburi hayo kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi ,kufuatia
kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania , Mhe. Kassim Majaliwa
kutaka makaburi na mnara yajengwe ili kuendelea kuwaenzi marahemu.
Aidha, Lukuba,
amemuagiza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Juma Gwisu kwenda
na kasi zaidi ya kukamilisha ujenzi wa
Makaburi hayo pamoja na mnara.
“Huu ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu , Mhe.
Kassim Majaliwa, alivyokuja Manispaa yetu kutembelea makaburi kwa mara ya kwanza ambapo aliagiza tuboreshe na tuanze ujenzi wa makaburi pamoja na mnara
mkubwa ambao utakuwa na majina yote ya marehemu kama moja ya njia za kuwaenzi,
uzio tayari tumemaliza kujenga, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro , Eng.
Emmanuel Kalobelo ameshatupatia fedha kupitia mfuko wa maafa zilizokusanywa kwa
ajili ya marehemu hawa, kwahiyo ujenzi umeanza , kikubwa niwaombe ndugu, jamaa
na marafiki wa marehemu wazidishe maombi wanapokwenda katika nyumba za ibada" Amesema Lukuba.
Hata hivyo, amesema katika ujenzi huo , litatengwa eneo rasmi
litakalo tumika kwa ajili kufanyia sala
na maombi kwa marehemu wote .
“Licha ya kuboresha makaburi lakini kutokana na
uzito wa eneno, tumeona tutenge eneo la kufanyia sala na maombi, eneo hili dini
zote watakaa na kila mtu ataomba kwa mujibu wa taratibu za dini yake , nizidi kuwaomba
ndugu wa marehemu tuwe wavumilivu katika
kipindi hiki kigumu, kuondokewa na ndugu zetu kusitufanye turudi nyuma kikubwa
ni kuwaombea na kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya familia zetu na maendeleo
yetu tunatambua marehemu wameacha watoto, familia na tegemezi lakini yote ni
mipango ya Mungu kila mtu atapitia njia hiyo muda na wakati ambao Mwenyezi
Mungu atamuhitaji” Ameongeza Lukuba.
Lukuba, amesema mara baada ya ujenzi huo kukamilika
, kutakuwa na utaratibu wa maadhimisho
ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wote kila mwezi wa 8, tarehe 10 ambapo
ndipo tukio la ajali ya moto lilitokea.
Ikumbukwe kuwa, mkasa
huo ulitokea majira ya saa mbili asubuhi ya Jumamosi baada ya lori lilibeba
shehena ya petroli kuanguka katika mji wa Morogoro, na watu kuanza kuchota
mafuta yaliyomwagika kisha mlipuko mkubwa kutokea.
Naye Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Juma Gwisu, amesema
ujenzi wote wa makaburi, fensi pamoja na mnara utagharimu kiasi cha shilingi
Milioni 35 na mradi huo unatarajiwa kumalizika Juni 10,2020.
Post a Comment