Header Ads

DC Chonjo awacharukia vikali Walanguzi wa Sukari Manispaa ya Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, akifungua kikao cha wafanyabiashara cha majadiliano juu ya kupanda kwa bei ya Sukari.


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga , akitoa maelekezo katika kikao cha Wafanyabiashara cha majadiliano juu ya kupanda kwa bei ya Sukari Manispaa ya Morogoro.
Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro (DAS), Ruth John (kushoto) akiwasalimia Wafanyabiashara mara baada ya kikao hicho kufunguliwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akitoa maelekezo kwa wafanyabiashara na Watendaji 

Afisa Utumishi Manispaa ya Morogoro, Waziri Kombo, akifuatilia kwa umakini kikao cha wafanyabiashara cha majadiliano juu ya upandaji wa bei ya Sukari.
Afisa biashara Manispaa ya Morogoro, Herman Festus, akitoa ufafanuzi  kufuatia kugundua kuwepo kwa ulanguzi wa Sukari kwa baadhi ya wafanyabiashara. 

Wafanyabiashara wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo,  katika kikao cha majadiliano juu ya kupanda kwa bei ya Sukari.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo,
 amewataka Wafanyabiashara wa Sukari Manispaa ya Morogoro kuacha tabia ya Ulanguzi wa Sukari badala yake wafuate sheria na muuongozo uliotolewa na Bodi ya Sukari Tanzania ya kutokuuza bei juu tofauti na bei elekezi ya sh2,700 kwa kilo.



Chonjo ameyasema hayo leo Mei 7, 2020 kwenye kikao alichokiitisha dhidi ya Wafanyabiashara wa Jumla na rejareja kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Chonjo, amewaagiza maofisa biashara na maofisa watendaji wa kata na vijiji wanapaswa kufuatilia  wafanyabiashara hao na kuwachukulia hatua za kisheria ambao bado wanaopandisha bei ya sukari.

Amesema licha ya kuwa na hali ngumu ya upatikanaji wa Sukari lakini Kiwanda cha Mtibwa na Kilombero walishapewa vibali vya kuagiza Sukari nje cha kushangaza badala ya  kuuza hapa Morogoro wao wanauzia Dar Es Salaam.

Amesema kuwa  serikali imeshatangaza bei elekezi ya sh2,700 hivyo wafanyabiashara watakaoendelea kuuza bei ya juu tofauti na hiyo wanatakiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Nimewaita hapa tujadili kwa pamoja katika suala hili la baadhi ya wafanyabiashara kuuza Sukari tofauti na bei elekezi , najua mwaka huu mvua zimenyesha sana na zao la Sukari linahitaji mvua za kiwango chake zikizidi sana hata uzalishaji wake unakuwa chini , lakini wananchi wa hapa Manispaa ya Morogoro  wamefikisha malalamiko yao ofisini kwangu kuwa bado kuna wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya juu ya sh2,700 , nimeona tuitane tuone nini tatizo na tuangalie hatua za kuchukua lakini kikubwa zaidi niwaombe wafanyabaishara hali ni ngumu sote tuna jua hivyo kuuza tofauti na bei elekezi ni kinyume na Sheria za Bodi , tujitahidi sana kuangalia hili, ukijiona wewe ni mfanyabiashara wa rejareja hupaswikuuza kama mfanyabaishara wa jumla , zingatieni  maagizo ya Serikali hawa maofisa biashara hawana hata huruma wao wakija wanakubeba na kukuchuklulia hatua” Amesema Chonjo.

“Niongeze kwa kusema wakati huu ndugu zetu Waislamu wapo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na wanakitumia kiungo hicho muhimu katika vyakula vyao , sasa ifike wakati tuone aibu pia tukizidisha hiyo bei mnategemea hali itakuwaje? Niwaombe fuateni sheria hili ni la mpito nitalifikisha kwa Mkuu wa Mkoa tuone tunalifanyaje lakini kubwa fuateni bei elekezi ili muendane sawa na Serikali pamoja na kurahisisha upatikanaji wa kiuno hicho adhimu kabisa kiweze kupatikana  kwa uarahisi” Ameongeza Chonjo.

Aidha , amsema kuwa  mfanyabiashara yeyote atakayekwenda kinyume na maagizo ya serikali akichukuliwa hatua za kisheria asilaumu kwani atakuwa amekiuka  utaratibu ndiyo sababu akafuatiliwa.

 Chonjo ameshauri kuwa Sukari  kwa Kilo Moja iweze kuuzwa kwa bei ya Shilingi  2700 hadi 2800, Mtibwa Sugar waweke kituo cha mauzo Morogoro, lakini wakati wa uzalishaji na kabla ya kiwanda cha Mtibwa hakijafungwa waweke mgao wa Sukari utakao wafanya wafanyabiashara kutofuata Sukari nje ya Mkoa ili bei ya Sukari iwe rafiki kwa wateja.

Pia, Chonjo, amewaomba Wafanyabiashara hao kuweza kuisaidia Serikali kuwabaini  walanguzi wa Sukari ambao wanaweza kuwatia doa na kuwachafulia  wafanyabaishara wengine.

Ameendelea kuwakumbusha wananchi waendelee kufuata ushauri wa Wataalamu wa afya juu ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA, huku akiwataka Wazazi kuendelea kuwalinda watoto kutozurua hovyo kufuatia  tamko la Serikali la kuzifungia Shule kwa muda katika mapambano dhidi  ya Ugonjwa wa CORONA.

Mwisho , amewataka Wafanyabishara kuacha kuchezeana rafu za kibiashara  kwa ni kumezuka baadhi ya wafanyabiashara kununua bidhaa hiyo ya Sukari dukani halafu utamkuta mbele ya duka hilo anauza kwa bei ya juu tofauti na alivyonunua kitu amabcho amepiga marufuku na kama watawakuta  watu wanafanya mchezo huo watasombwa wote na kuchkuliwa hatua kali za kisheria.

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewaomba wafanaybishara kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito kwa kuuza Sukari hiyo kwa bei elekezi ya Serikali licha ya kuwepo kwa ugumu wa upatikanaji wake .

Kihanga , amesema  kipindi  hiki hali ni ngumu sana kwa wafanyabiashara hata kwa wananchi ukizingatia kuna janga la Ugonjwa wa CORONA ambalo limechangia kudolola kwa biashara lakini amewataka wafanyabishara janga la CORANA lisiwe  kikwazo cha kuwakandamiza wananchi washindwe kumudu mahitaji yao ya kila siku.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,  ametoa onyo kwa wafanyabiashara wa sukari wa waliopo Manispaa ya Morogoro  wanaouza bei ya juu tofauti na maelekezo ya serikali.

“Wanaoendelea kuuza sukari kwa sh3,500 kwa kilo mnajitafutia matatizo kwani serikali itawachukulia hatua, uzeni kwa bei inayotakiwa , kama Bodi ya Sukari ilivyopanga na siyo vinginevyo,” amesema Lukuba.

Kwa upande wa Afisa Biashara wa Manispaa ya Morogoro, Festus Herman , amesema waligundua kuwepo kwa ulanguzi wa bei ya sukari  mara baada ya kufanya  ziara  ya kushtukiza kwenye baadhi ya maduka na kubaini kuwa kuna ulanguzi unaofanyika kwa wafanyabiashara ambao wanauza Sukari tofauti na bei elekezi ya Serikali.

Aidha, Festus ,amesema bei elekezi ya Wafanyabishara wa Sukari ikitoka Dar Es Salaam inachukuliwa kwa Shilingi 127,500/= kwa mfuko wenye Kilo 50 lakini ukifika Mkoani Morogoro mfuko huo huuzwa kwa Shilingi 130,000/=

Mmoja wa wafanyabiashara ambaye jina lake limehifadhiwa, amesema kupanda kwa bei ya Sukari kumetokana na bei wanayonunulia Sukari Jijini Dar Es Salaam kuwa kubwa hivyo kushindwa kuuza kwa bei elekezi kwa kuhofia hasara.


Amesema kuwa wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakinunua Sukari ya kilo 50 kwa Shilingi 127,500/= kutoka Dar Es Salaam, lakini wakifikisha Morogoro wanauza kwa Shilingi 129000/= hivyo inawalazimu wao kuwauzia bei ya juu na wanalazimika na wao kuongeza bei ya Sukari tofauti na bei elekezi.

“Mimi nilifuatwa na kukamatwa na kulala mahabusu, niliambiwa kuwa kosa langu ni kuuza Sukari kwa bei ya Shilingi 3000 kwa kilo , lakini bado kuna changamoto , ukiangalia mimi ni mfanyabiashara wa rejereja bei ya Mfuko mmoja wa Sukari wa Kilo 50 tunauziwa shilingi 127,500/= hapo hujatoa pesa ya ushushaji na ya usafiri , sasa tulichokuwa tunaiomba Serikali ianagalie uwezekeano wa sisi kuuza kwa bei kidogo ili tufidie gharama ambazo tunazipata japo kweli hali ya Sukari na upatikanaji wake imekuwa ngumu”” Amesema mfanyabiashara huyo.




No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.