MKURUGENZI MANISPAA YA MOROGORO AWATAKA WATUMISHI KUWEKA MALENGO KATIKA UTENDAJI WA KAZI.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro akifungua semina ya mafunzo ya OPRAS kwa Watumishi kwenye Ukumbi wa Manispaa. |
Afisa Utumishi Manispaa ya Morogoro , Waziri Kombo, akitoa maelekezo kwa Watumishi wakati wa Semina. Afisa Utumishi akiendelea kutoa maelekezo kwa Watumishi. |
Washiriki wakiwa makini kusikiliza mafunzo.
MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewataka Watumishi wa Manispaa ya Morogoro kuweka malengo katika Utendaji wa kazi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi na kuiletea maendeleo Manispaa na Taifa kwa ujumla.
Hayo ameyasema wakati wa kuzindua mafunzo kwa Watumishi pamoja na Watendaji wa Kata kuhusu mfumo wa wazi wa mapito na tathmini ya Utendaji kazi wa Watumishi wa Umma (OPRAS) yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Amesema kuwa mafunzo hayo yanaendeshwa kwa njia za majadiliano, maswali na majibu , pamoja na kubadilishana uzoefu .
Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo , Lukuba, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki kujadili maana, umuhimu na namna mfumo wa wazi wa mapito na tathmini ya Utendaji kazi wa Watumishi wa Umma (OPRAS) kwa watumishi wa Umma unavyofanya kazi , kuwawezesha watumishi ambao ni wasimamizi wa kazi kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kuweka malengo ya utendaji kazi na kuwasimamia watumishi waliopo chini yao katika kuweka malengo ya utendaji kazi , kuwawezesha washiriki kwa vitendo katika kuweka makubaliano ya utendaji kazi , kufanya mapitio ya utendaji kazi ya nusu mwaka na upimaji wa utendaji kazi wa mwaka pamoja na kuongoza majadiliano ya watumishi kuhusu changamoto zao za kiutendaji kazi na mbinu za kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Amesema kuwa uanzishwaji wa OPRAS ni hatua muhimu kwa serikali katika kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma kwa umma.
Aidha, amesema OPRAS ni chombo muhimu cha uwajibikaji kwa kila mtumishi ambacho kinasisitiza umuhimu wa USHIRIKISHWAJI, UMILIKI NA UWAZI ambapo watumishi wanahusisha katika kupanga malengo, utekelezaji, kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa malengo na mchakato wa kufanya mapitio ya utendaji.
Lukuba amesema baada ya mafunzo hayo anatarajia kuwa watumishi wataweza kueleza maana , umuhimu na kanuni za usimamizi wa utendaji kazi (Performance Management ) katika utumishi wa Umma, kuonesha uelewa mpana juu ya mfumo wa wazi wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi , kuonesha uelewa mpana wa kanuni za maadili katika utumishi wa Umma na kuzitekeleza kwa Vitendo katika maeneo yao ya kazi , kubuni njia bora za utoaji wa huduma kwa wananchi na Watumishi wanaowasimamia kwa ufanisi na uadilifu pamoja na kuonesha uelewa na ubunifu katika utunzaji na matumizi ya kumbukumbu kwa ajili ya kufanya maamuzi mbalimbali.
Mbali na usimamizi wa utendaji kazi lakini matokeo ya mfumo huo ni mawasiliano ya mara kwa mara kati ya msimamizi wa kazi na mtumishi, na uelewa wa pamoja wa mahusiano yaliyopo kati ya malengo ya taasisi na yale ya mtumishi binafsi.
“Tumefungua rasmi mafunzo haya kwa watumishi wenu nafikiri kile ambacho kitafundishwa kitawasaidia sana katika utendaji wao wa kazi , lengo tunataka kuona matokeo chanya , Mabadiliko haya ya kutathmini utendaji kazi wa watumishi wa umma yanakwenda sambamba na sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 na Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 ambazo zote zinasisitiza uwekaji wa mifumo ya menejimenti ya utendaji bora wa kazi inayojali matokeo ya kazi na kwamba maswala ya ajira, uteuzi na kupandishwa ngazi katika utumishi wa umma yatakuwa kwa ushindani uwazi na unaozingatia sifa, ujuzi na uadilifu wa hali ya juu” Amesema Lukuba.
Mwisho, amesema mategemeo yake ni kwamba mwongozo huo wa OPRAS utatumika kama chombo cha watumishi katika taasisi za umma kujifunza jinsi ya kutumia na kutekeleza OPRAS kwa nia ya kuwa watendaji wanaojali zaidi matokeo bora katika utoaji wa huduma kwa umma.
Kwa upande wa Afisa Utumishi wa Manispaa ya Morogoro, Waziri Kombo, Ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa OPRAS unaeleweka kwa pande zote za mwajiri na mwajiriwa, Manispaa ya Morogoro kupitia muongozo wa Serikali imefungua mafunzo haya kuhusu utekelezaji wa OPRAS katika Utumishi wa Umma.
Kombo amesema kuwa, mwongozo huu unatoa tafsiri ya maneno yatumikayo mara kwa mara na unatoa maelezo ya jinsi ya kujaza fomu ya OPRAS na jinsi ya kufanya mapitio na mwisho jinsi ya kutumia matokeo ya mapitio na tathmini ya utendaji kwa mfano utoaji wa zawadi, adhabu na hatua za maendeleo kwa nia ya kuboresha utendaji wa mtumishi.
Katika hatua nyengine, Kombo, amewataka Watendaji wa Kata kupitia katika maeneo ya biashara, maduka na vibanda pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watu ili kuona kama watu wanafuata maelekezo ya wataalamu wa afya katika kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Naye Mwalimu wa mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Cliford Ringo, amewaomba watumishi kusikiliza kwa uumakini kwa kuwa wao ndio Viongozi wa ngazi za juu hivuo wasipo kuwa na uelewa mkubwa itakuwa vigumu kwenda kuwafundisha wengine huko waendapko na kupelekea mfumo huo kuonekana mgumu.
Akitoa maada katika Mafunzo hayo, Dk. Ringo, amesema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali katika matumizi ya OPRAS kwa Watumishi wa Umma kitu kinachopunguza ufanisi katika kufikia malengo ya kazi.
Dk. Ringo, amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kutokana na changamoto zilizobainishwa ikiwamo kutokuwepo kwa uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa OPRAS kwa Watumishi wa Umma , kutokuwepo kwa usimamizi thabiti katika kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa kama inavyotakiwa pamoja kutokuwepo kwa taratibu madhubuti katika kufanya ufwatiliaji na tathmini.
Mbali na changamoto alizozitaja amesema kuwa changamoto nyingine iliyobainishwa ni suala la ujazaji wa fomu ya OPRAS hususan katika kuweka sahihi wa malengo ya mtumishi unaoshabihiana na upimaji sahihi wa utendaji wa kazi.
Post a Comment