Header Ads

DC Chonjo awataka Madiwani Manispaa ya Morogoro kuzingatia maadili ya kazi katika utendaji wao.



Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, akifungua mafunzo ya maadili kwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Kigurunyembe.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo,akisoma taarifa wakati wa uzinduzi wa mafunzo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, akitoa neno la shukrani baada ya uzinduzi wa mafunzo. (kulia) ni Afisa Maadili kutoka Secretarieti ya Maadili Kanda ya Mashariki Morogoro na Tanga , Selemani Shabani, 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akitoa utambulisho kabla ya uzinduzi wa mafunzo kuanza.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro Mjini, Sofia Kibaba, akitoa salamu za Chama wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya maadili kwa Madiwani.

Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro wakiwa Ukumbini wakiendelea na Mafunzo  ya Maadili kwenye Ukumbi wa Chuo Cha Ualimu Kigurunyembe.

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amewataka Madiwani wa Manispaa ya Morogoro kuzingatia maadili ya kazi katika utendaji wao ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kauli hiyo ameitoa leo Mei 19, 2020 wakati akizindua mafunzo ya Maadili kwa Madiwani wa Manispaa hiyo ,yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Kigurunyembe.

Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema semina hiyo ya mafunzo ya maadili ni somo muhimu kwa maisha ya kawadia na katika utendaji wao wa kazi katika kuwaongoza wananchi na kutoa huduma.

Amesema kiongozi asiyezingatia maadili kazini hata katika utendaji wake unakuwa na shida kutokana na kukosa misingi ya uadilifu ambayo ndiyo nguzo kuu ya utendaji kazi.

DC Chonjo ,amesema miongoni mwa vitendo  ambavyo vinasababisha kukosekana kwa uadilifu kazi ni pamoja na kupokea na kutoa rushwa, ubadilifu wa mali za umma, kuwa na mahusiano wa kimapenzi baina ya wafanyakazi wenyewe, kutumia cheo kwa maslahi binafsi, mgongano wa maslahi, tabia ya ulevi , uasherati na ugomvi kwenye jamii  ambapo vitu vyote hapo  vinamuondolea sifa kiongozi kimaadili.

Aidha, amewaasa Madiwani watako fanikiwa kurudi tena katika awamu ijayo ya uongozi baada ya uchaguzi waendelee kuzingatia ahadi ya uadilifu kwa kujaza na kusaini hati ya uadilifu .

“”Viongozi lazima tuwe waadilifu, hata Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Magufuli , amekuwa mfano kwa kujaza na kusaini hati ya uadilifu inayosimamiwa na tume ya maadili na viongozi wa Umma na viongozi wote tulioteuliwa tumekula kiapo hicho , kwahiyo tutambue kazi zote tunazo zifanya  kwa wananachi wetu ni kwaniaba ya Mhe. Rais kwa kufuata maudhui na maadili kama Rais wetu anavyofanya, niwaombe sana mzingatie maadili lakini matarajio yangu ni kwamba baada ya uchaguzi huu wote  kwa kuwa mmefanya maendeleo makubwa katika Kata zenu na Manispaa yenu  na mtakula kiapo cha maadili “ Amesema DC Chonjo.

Amesema kuwa ,  kanuni za mgongano wa maslahi za mwaka 2020 zimeelezea ni kwa namna gani viongozi wa umma  wanapaswa kujiepusha na mgongano wa maslahi mfano katika kuweka mashinikizo katika maamuzi  yenye mgongano wa maslahi kama vile kwenye bodi za tenda zinazopitishwa katika Halmashauri kwa kutaka Kampuni Fulani ipewe tenda ambapo kampuni husika ina maslahi na kiongozi anayeshinikiza.

Amesema kuwa matarajio yake baada ya mafunzo hayo madiwani watakuwa  wameweza kupata maarifa ya kimkakati hususani kwa wale wenye dhamira ya kugombea .

Katika hatua nyengine, amesema wanaelekea katika Uchaguzi  Mkuu hivyo kuna haja ya viongozi kufanya tathmini tangia walivyochaguliwa na kuingia madarakani mwaka 2015 mwaka 2020 ni mambo gani wamewafanyia wapiga kura wao , malengo ya kisiasa waliyokuwa nayo kama kiongozi na vitu gani wanatakiwa kufanya ili waendane na mabadiliko ya wapiga kura wanavyohitaji  huku ukiwa unaendelea na kasi ya Mkuu wa nchi.

‘””Naamini kabisa wakati huu sitasikia kuna Diwani anatembeza kanga, shilingi 10000 wala 2000, skafu za chama n.k, kwa sababu mmeshaambiwa anayetoa na anayepokea wote ni wakosaji , lakini nipende kuwatia moyo kwa kazi mlizozifanya kama mtajipanga mnaweza kurudi kama mlivyo, kikubwa mnatakiwa mtoe taarifa kwa wananchi wenu kuhusu mambo yaliyofanywa na Serikali katika Kata zenu ,tunajua hiki ni kipindi cha CORONA lakini ujanja kichwani, mnaweza kufanya mikutano midogomidogo inayoruhusiwa kama kuwaita wajumbe wa mitaa mkawafafanulia mliyoyafanya ,au kukaa na wazee maarufu ama viongozi wa dini na CORONA itakapokwisha hata ukiitisha mikutano mikuu hapo utakuwa umejenga misingi imara na kazi itakuwa nyepesi sana , fanyeni hivyo lakini msitoe rushwa “ Ameongeza DC Chonjo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewaomba Madiwani kuwa wasikivu kwani watoa mafunzo wamekuja na wanajua nini ambacho wanatakiwa kuwasaidia .

‘’Ni mafunzo mazuri upande wetu, hii sio mara ya kwanza lakini tunakumbushwa zaidi ili kuendana na mabadiliko ya uongozi uliopo madarakani ambapo uanataka kila kiongozi awe na maadili kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wake” Amesema Mhe. Kihanga.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewapongeza madiwani pamoja na Wakufunzi kwa kukubali kufanya semina hiyo huku akiwakumbusha na kuwaomba  Madiwa kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia Maadili ,  kanuni na taratibu za nchi kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Nawashukuru sana wageni wetu kutoka tume ya Secretarieti ya maadili Kanda ya Mashariki Morogoro na Tanga , kwa kutukubalia kuendesha mafunzo yetu, naamini baada ya mafunzo haya tunategemea Madiwani wetu wataendesha kazi zao kwa kuzingatia maadili katika utoaji huduma kwa wananchi wao”” Amesema Lukuba.

Kwa upande wa Afisa Maadili kutoka Secretarieti ya Maadili Kanda ya Mashariki Morogoro na Tanga , Selemani Shabani, amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kutokana na  changamoto mbalimbali katika upande wa maadili kwa Watumishi wa Umma  kitu kinachopunguza ufanisi katika kufikia malengo ya kazi.

Mbali na mafunzo amesema Madiwani watakaopita awamu ijayo baada ya uchaguzi kumalizika watajaza na kusaini hati ya uadilifu kama ilivyo kwa viongozi wengine wa uuma.







No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.