Header Ads

Manispaa ya Morogoro yazindua kampeni ya usafi maeneo ya shule na makazi ya watu.

Wananchi wakiendelea na usafi wa kufyeka nyasi katika Shule ya Msingi  Mafisa ''A'' wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya usafi maeneo ya shule pamoja na makazi ya watu.
Afisa Tarafa wa Manispaa ya Morogoro, Winfred Kipako ,akifyeka nyasi pembezoni mwa barabara wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usafi wa maeneo ya shule pamoja na makazi ya watu.
Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana akifyeka nyasi katika eneo la Shule   wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usafi wa maeneo ya Shule pamoja na makazi ya watu.
Afisa Mazingira Manispaa ya Morogoro , Dauson Jeremia, akifyeka nyasi katika eneo la Shule   wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usafi wa maeneo ya Shule pamoja na makazi ya watu.

Kaimu Mtendaji Kata ya Mwembesongo , Mwaru Kizega (wapili kutoka kushoto) akijadili jambo na wananchi wakati wa uzinduzi  wa Kampeni ya Usafi wa maeneo ya Shule pamoja na makazi ya watu.


HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro, imezindua rasmi kampeni ya usafi na mazingira katika maeneo za shule pamoja na makazi ya watu.

Kampeni hiyo imezinduliwa leo Mei 16,2020 na Afisa Tarafa wa Manispaa ya Morogoro, Winfred Kipako kwenye Shule ya Msingi Mafisa ''A'' Kata ya Mwembesongo.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Kipako, amesema Manispaa imeamua kujiwekea utaratibu wa kuanzisha Kampeni hii ya usafi ambayo itakwenda moja kwa moja ikiwa na malengo  ya kumshirikisha kila Mwananchi anayeishi Manispaa ya Morogoro pamoja na Kata zote kuhakikisha anashiriki katika shughuli za usafi.

Amesema kuwa lengo la kuanza katika maeneo ya  shule ni kutokana na shule kukosa wanafunzi kufuatia likizo ya Serikali baada ya kuingia kwa Janga la ugonjwa wa CORONA , hivyo maeneo mengi ya shule yamegeuka vichaka jambo ambalo ni hatarishi kufanya maeoeno hayo kuwa kificho cha  wadudu wakali pamoja na kuweka mazalia ya mbu na kusababisha magonjwa kwa jamii kama vile Malaria.

Kipako , amesema kuwa  Manispaa ya Morogoro kupitia Idara ya Mazingira itaunda kikosi kazi ambacho kitaongozwa na Afisa Mazingira wa Manispaa kwa ajili ya kuendesha kampeni ya usafi kwa kupitia Kata moja badala ya nyengine.

“ Nimshukuru sana Mkurugenzi wetu wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba  kuja na wazo zuri sana  pamoja na Afisa Mazingira wetu wa Manispaa  kwa jitihada mbali mbali za kupambana na suala la usafi , baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wetu wa manispaa , tulikaa vikao tuka kubaliana na kushusha  maelekezo kwa Watendaji wote wa Kata  kwamba tunaanza Kampeni ya usafi , kubwa zaidi nimefurahishwa sana kuona kampeni hii wananchi wameipoke kwa bashasha sana , nawapongeza sana Watendaji wa kata , watendaji wa Mitaa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa hapa Mwembesongo kwa uhamasishaji wao ambapo tumeona wananchi, kamati za shule, walimu wa shule ,  wameitikia wito na  kutuunga mkono, hatutaishia hapa leo tumezindua na tunatarajia kampeni hii kuwa ya kipekee kwani imezingatia maeneo  yote yaliyopo ndani ya Manispaa tuendelee kushikamana kwa pamoja tutafanikiwa na Manispaa yetu itakuwa ya mfano kwa usafi ‘’ Amesema Kipako.

‘’Kampeni hii tutafika nyumba kwa nyumba, Mtaa kwa mtaa, Kata kwa Kata , na wale  ambao watashindwa kuendana na kasi ya usafi wa Mazingira ndani ya Manispaa yetu iwe wananchi au watendaji watachukuliwa hatua kali  za kisheria kwa kushindwa kufikia malengo, kikubwa wananchi wafanye usafi na waweke taka sehemu elekezi huku sisi kazi yetu ikiwa ni kupitia na kuzikusanya kuzipeleka dampo , tukishirikiana kwa pamoja changamoto ya usafi katika Manispaa yetu itabaki historia “” Ameongeza Kipako.

Hata hivyo, amewaagiza Watendaji wa Kata, Mitaa, Maafisa afya pamoja na wananchi waliopo  ndani ya Manispaa waibebe kampeni hii na kuichukulia kwa uzio wa hali ya juu sana katika maeneo yao ili yale malengo tarajiwa yaweze kutimia.

Amesema matarajio yake ni kuona Kampeni hiyo inafanikiwa kwa asilimia 100 ili yaendane na malengo yaliyokusudiwa katika kupata matokeo chanya yatakayoifanya Manispaa kung’ara katika suala zima la usafi ambalo limeonekana kuwa changamoto.

Kwa  upande wa Afisa Mazingira Manispaa ya Morogoro , Dauson Jeremia, amesema kampeni hiyo ya usafi italenga katika kusimamia mifereji yote inayozunguka biashara, soko, Viwanda, makazi ya watu, shule pamoja na ofisi ikiwemo ukaguzi wa nyasi ndefu katika  maeneo hayo.

‘’Tumezindua rasmi kampeni yetu ya usafi tukianza na maeneo ya shule, lakini hatutaishia hapa pia tutakuwa na operesheni ya kuangalia wale watu ambao wanaotupa na kumwaga  takataka katika mtaa, mtaro wa maji ya mvua, uchochoroni au mahali popote hadharani au katika eneo lolote la wazi bila idhini ya Halmashauri na kuweza kuwachukulia hatua kali za kisheria “ Amesema Jeremia.

Amesema kampeni hiyo itakuwa na malengo ya kumshirikisha kila Mwananchi anayeishi Manispaa ya Morogoro pamoja na Kata zote kuhakikisha anashiriki katika shughuli za usafi.

Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Mwembesongo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya mipango miji Manispaa ya Morogoro, Mhe. Ally Kalungwana, ameipongeza Manispaa kwa kuja na wazo zuri ambalo linaweza kuwa suluhisho la changamoto ya usafi ndani ya Manispaa.


Amesema Kampeni hiyo wao wameipokea vizuri sana , na watahakikisha wanakuwa bega kwa bega ili kuona inafanikiwa na inazaa matunda.

Kalungwana , ametoa wito kwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro kuichukulia kampeni hiyo kama suluhisho la usafi ndani ya Manispaa na kuendelea kuhamasisha wananchi waweze kushiriki kikamilifu ili malengo yaliyotarajiwa  yaweze kufikiwa.

“Tumeipokea vizuri sana kampeni hii, ni jambo zuri na la kiubunifu, nampongeza Mkurugenzi wetu anafanya kazi kubwa sana, idara ya mazingira na vikundi vya usafi,  niwaombe wananchi wa Kata yangu tuipokee kwa uzito mkubwa na tushirikiane kikamilifu kwa ajili ya kuweka Kata yetu safi , nawapongeza sana wananchi walioitikia wito na kuja kutuunga mkono na tutashinda vita hii ya usafi na kuifanya Manispaa yetu isonge mbele” Amesema Mhe. Kalungwana.

Hata hivyo, amesema katika kipindi hiki ambacho  shule zimefungwa ni vyema wananchi wakajitokeza kufanya usafi katika maeneo ya shule ili ziendelee kuwa  na mazingira  mazuri ili hata shule zikifunguliwa wanafunzi wasiingie katika adha kubwa ya kuminyana na mapori. 

Naye mkazi wa Kata ya Mwembesongo, Bi. Sawita Haji Narani, amesema wao wameipokea kampeni hiyo kwa kishindo kikubwa sana na kuahidi ushirikiano mkubwa dhidi ya Serikali katika kusimamia usafi.
























No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.