MEYA MANISPAA MOROGORO ATAKA MIRADI IKAMILISHWE KWA WAKATI.
Mstahiki Meya Manispaa Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga akifungua kikao cha Baraza la Madiwani. |
Mstahiki Meya Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu, Mhe. Pascal Kihanga, ameitaka Miradi yote inayotekelezwa kwenye Manispaa ya Morogoro hususani miradi ya Soko Kuu la Kisasa na Stendi mpya ya Daladala Mafiga imalizike kwa wakati.
Hayo ameyasema Aprili 30,2020 kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Kihanga , amesema wananchi wanasubiri miradi yao wamekaa muda mrefu kwenye maeneo ambayo siyo rasmi.
" Tunaomba miradi hii ikamilike haraka, tumewavumilia sana wakandarasi, Manispaa yetu ni sikivu mno lakini ifike wakati tuseme inatosha, Masoko ambayo tumewaweka wafanyabiashara wetu siyo rafiki sana ukizingatia kipindi hiki cha ugonjwa Wa Corona hata tunavyokwenda kuwahamasisha wasipange Vitu chini je tunawapeleka wapi? Hata Stendi yetu imejaa kwa sasa Magari ni mengi mpaka yanasababisha msongamano wawatu na sisi hatutaki msongamano huo , tunawaomba wakandarasi waharakishe ili ukifika muda tuliowapa watukabadhi miradi hiyo tuipeleke kwa wananchi " Amesema Kihanga.
Aidha, Kihanga, ametaka taarifa ya matumizi ya hela itakayobaki katika Ujenzi wa Stendi mpya ya Daladala Mafiga,baada ya kuwa wamepunguza baadhi ya vitu ili itumike kujenga vioski kitu ambacho ni hitaji la wananchi
Katika hatua nyengine amelipongeza Baraza la Madiwani pamoja na Mkurugenzi Wa Manispaa, Sheilla Lukuba, kwa maamuzi ya kufufua upya ujenzi wa Stendi ya Kaloleni baada ya kupata Mkandarasi mpya Nandhra Engineering aliypewa Mkandarasi hiyo kwa muda muda wa miezi 2 sawa na siku 60.
Amesema huo ni uamuzi mzuri kwani mradi huo unakwenda kuongeza chanzo chengine cha Mapato na kuifanya Manispaa kutotegemea Fedha za Ruzuku kutoka Serikalini . .
Lakini kubwa amemtaka Mkandarasi aliyekabidhiwa Mradi huo kwenda na kasi inayotakiwa na kukamilisha ujenzi huo kwa wakati. " Nandhra Engineering tumewakabidhi mradi huu kwa vile tunafahamu uwezo wenu, msifanye ubabaishaji kama wenzenu, mlianza vizuri miradi yetu ya Soko na Stendi Mafiga na sasa hii ni fursa nyengine mmeipata itendeeni haki ili muweze kupata tenda nyengine ndani na nje ya Manispaa yetu" Ameongeza Kihanga.
Hata hivyo ameendelea kutoa rai kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuendelea kufuata ushauri wa Wataalamu wa Afya katika kujikinga na Ugonjwa wa Corona ikiwemo kunawa Maji tiririka na sabuni, kutumia Vitakasa mikono ( Sanitizer), pamoja na kuepuka msongamano isiyo ya lazima na kukaa nyumbani kama mtu hana sababu ya Msingi ya kutoka
Mwisho amechukua nafasi ya kutoa pole kwa niaba ya Baraza la Madiwani kufuatia kifo cha aliyekuwa Naibu Meya Manispaa Morogoro na Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Mhe. Isihaka Sengo huku akiwataka Wanafamilia, Ndugu pamoja na Marafiki kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha mpito .
Post a Comment