Header Ads

MADIWANI MANISPAA YA MOROGORO WAMPONGEZA MKURUGENZI KWA KUANDAA SEMINA YA MAADILI YENYE KULETA CHACHU YA UWAJIBIKAJI KWA WANANCHI.

Waheshimiwa Madiwani wakiwa katika Semina ya Maadili iliyoandaliwa  na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro katika kuwajengea uwezo watendaji pamoja na kuleta chachu ya uwajibikaji kwa wananchi katika utoaji wa huduma bora. 

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, wamempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,  kwa kuwaandalia Semina ya mafunzo ya  Maadili  yenye kuleta chachu ya uwajibikaji kwa Wananchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofautitofauti, Madiwani hao wamesema mara baada ya semina hiyo kumalizika watakuwa wamejifunza mambo mengi , ikiwemo uwajibika kwa wananchi na kutoa huduma bila ya upendeleo na namna ya kuishi na Watumishi na kutengeneza timu moja kwa ajili ya Maendeleo ya Manispaa.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga,amesema katika mambo waliyojifunza ni pamoja na kutojihusisha na rushwa, na viashiria ambavyo vitamfanya mtu kujulikana amekula rushwa.

Kihanga , amesema kuwa Madiwani wamekuwa wakikumbana na changamoto ya namna hiyo ambapo wanaweza wakafikiri sio rushwa kumbe wametengeneza mazingira ya rushwa na kuwaweka matatani.

“ Mkurugenzi wetu amefanya jambo la maana sana, tumepata uelewa mkubwa sana katika semina hii hususani katika uwajibikaji, lakini jinsi ya  kujaza fomu ya maadili pamoja na kusaini hati ya uadilifu ambayo ni muhimu sana haswa kipindi hiki ambapo tumebakiza muda mchache tuwe uraiani , lakini mafunzo haya hayatusaidii tu tukiwa katika Uongozi bali hata uraiani ili kujua heshima yako ikoje kwa jamii “ Amesema Mhe. Kihanga.

Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana, amesema hii ni mara ya pili kukutana nayo mafunzo ya namna hiyo lakini kwa awamu hii mafunzo hayo yameiva vizuri sana .

“ Tunamshukuru sana Mkurugenzi, mafunzo ya awamu hii yamekuwa mazuri sana, maana tumewaza kufahamu nini maana ya maadili, kushirikiana na wataalamu wa Manispaa na kuwaona kama ndugu zetu na namna ya kushirikiana nao , lakini kubwa zaidi tumepata kujua jinsi ya  uongozi kati ya Diwani na Watumishi wa Serikali” Amesema Mhe. Kalungwana.

Naye Diwani wa Kata ya Boma, Mhe. Amiri Nondo, amesema mafunzo hayo yamewasaidia sana kujua namna ya kuwasiliana na jamii.

“ Mafunzo haya siyo mara ya kwanza kuyapata lakini yamekuwa yakipee kwa kuwa tumejifunza na kufahamu juu ya kanuni mpya za maadili na Uongozi ikiwemo namna ya kujiandaa na kuapa na kutimiza  kwa kayaishi juu ya viapo katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika Serikali na kuona namna gani haki inatendeka kwa jamii “ Amesema Mhe. Nondo.

 Kwa upande wa Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Scolastica Mkude, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuweza kupata mbinu za kuweza kupambana.

“Nilikuwa na matarajio ya kubakia katika Viti maalum, lakini kutokana na mbinu nilizozipata kwenye mafunzo, sitabaki tena kwenye Viti Maalum badala yake nitakwenda kupambana kwenye Kata kwakuwa nia ninayo na mafunzo niliyoyapata yataweza kunisaidia sana” Amesema Mhe. Scolastica.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.