WAZAZI WATAKIWA KUSIMAMIA NIDHAMU YA WATOTO
MWAKILISHI wa Mkurugenzi wa Vipindi vya Planet FM Morogoro ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ladies Talk Tanzania, Salome Sengo, amewataka wazazi kusimamia ipasavyo maadili ya watoto wao ili waweze kufanikiwa na kufikia malengo waliyojiwekea kitaaluma.
Sengo, amewataka Wazazi kushirikiana na walimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa na nidhamu ya kuridhirisha katika jamii inayowazunguka.
Kauli hiyo ameitoa, Septemba 01/2023 katika mahafali ya kuwatunuku vyeti wanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Msingi Misufini B Kata ya Mafiga, Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Sengo, amewataka walimu na wazazi kuhakikisha wanawasisitiza wanafunzi kutii sheria za shule kama vile uvaaji wa sare sahihi ya shule, kuheshimiana na utumiaji wa lugha nzuri.
“Wazazi tuna jukumu kubwa la kusimamia suala la maadili ya watoto wetu. Hili ni suala ambalo huwezi kulitenanisha na mafanikio bora kitaaluma, mara nyingi mtoto mwenye nidhamu na maadili mema daima hufanya vizuri darasani na yule asiye na nidhamu huporomoka katika taaluma, nasisitiza nidhamu na taaluma huenda pamoja, haiwezekani kuvitenganisha hata mara moja.”Amesema Sengo.
Hata hivyo, amewataka wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba kujiandaa vyema kufanya Mitihani yao inayotarajiwa kuanza hivi karibuni na kujitahidi kutulia na kutumia vyema maarifa yote waliyopata kutoka kwa walimu wao.
Pia,amewakaumbusha kwamba watakapomaliza mitihani yao wasijisahau na kufikiri kuwa sasa elimu ndio basi bali watambue kuwa safari ya kutafuta elimu ndio inaanza.
Naye Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile, amewataka wazazi kuhakikisha wanawatengea muda wanafunzi katika kujiandaa kwa masomo ya sekondari mara wanapomaliza mitihani yao ya darasa la saba.
"Nawasihi muwe raia wema wenye kuwajibika katika jamii yote. Maisha sio lele mama! wekeni juhudi katika masomo, elimu ndio msingi bora wa maisha, msidanganyike hakuna njia ya mkato katika kufanikiwa katika maisha".Amesema Mhe. Butabile.
Butabile ,amesema kuwa Waalimu wanatakiwa kutambua kuwa shughuli za kila siku shuleni zinahitaji juhudi za hali ya juu.
Aidha, Butabile, amewataka wanafunzi wanaobaki shuleni kujitahadi kuzingatia Masomo kwani walichonacho shuleni ni kifupi sana, lakini ni kipindi muhimu sana katika kuandaa maisha yao ya baadaye.
Hata hivyo, Butabile, amewataka wanafunzi kuwasikivu, kutii sheria za shule, tekeleza majukumu yao wanayopewa katika masomo, kuepuka vitendo viovu katika jamii pamoja na kuwa na nidhamu inayopendeza machoni na mioyoni mwa wazazi, walezi na walimu wao.
Naye Afisa Elimu, Vifaa na Takwimu ambaye pia ni Mlezi wa Kata ya Mafiga katika upande wa Shule za Msingi, Taaluma Msingi Manispaa ya Morogoro , Stephen Mkulia, amewataka Waalimu kuboresha zaidi utendaji kazi wao ili kufikia matarajio ya Ufaulu ambayo Halmashauri ya Manispaa yanatarajia.
Mkulia, amewasisitizia walimu kukabiliana na changamoto zinzojitokeza katika sekta ya elimu kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea, badala yake kuhakikisha wanapanga mipango yao, wanajiwekea malengo ya muda mfupi na mrefu na kubuni mikakati sahihi inayotekelezeka ambayo itawezesha kufikia malengo waliyojiwekea.
Aidha,amewashauri wazazi kutoa ushirikiano wa hali ya juu katika suala zima la kufanikisha matokeo mazuri ya ufaulu kuanzia madarasa ya awali, la kwanza hadi darasa la Saba.
"Yote haya yanawezekana pale tutakapotekeleza wajibu wetu wa kusimamia vyema yale yote wanayofundishwa watoto wetu wanapokuwa shuleni, watoto hupewa mazoezi mbalimbali (homework) na walimu wao ili wazifanye wanapokuwa nyumbani, ni jambo la msingi tukitenga muda kusimamia katika eneo hili. "Amesema Mkulia.
Post a Comment