Header Ads

KITUO CHA AFYA SABASABA MANISPAA YA MOROGORO CHAANZA KUTOA HUDUMA ZA UPASUAJI NA MIONZI



KITUO cha Afya Sabasaba Manispaa ya Morogoro kimeanza  rasmi kutoa huduma za upasuaji Septemba 13/2023 baada ya kumfanyia upasuaji mgonjwa mmoja.

Akizungumza juu ya Kituo hicho kutoa huduma za upasuaji, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ,Ally Machela, amesema huduma hiyo imeanza Septemba 13/2023  mara baada ya Kituo hicho kukamilika kwa vifaa tiba.

Machela, amesema kuwa kufuatia Kituo hicho kutoa huduma za upasuaji, kitasaidia  kuondoa msongamano wa wagonjwa wa upasuaji Hospitali Kubwa ya Mkoa.

"Tumepokea Vifaa kutoka TAMISEMI,tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani Manispaa yetu ya Morogoro tumekuwa wanufaika wakubwa wa  fedha kutoka Serikali Kuu katika huduma mbalimbali ikiwemo za afya ,mpaka sasa tumeimarisha miundombinu ya Zahanati zetu, Vituo vyetu vya afya, naamini wataalamu wangu sasa watakwenda kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi" Amesema Machela.

Aidha, Machela,amesema kukamilika kwa utoaji wa huduma za upasuaji anaamini huduma hizo zitatolewa kwa ufanisi zaidi zikiwemo huduma za dharura na kufanya upasuaji hasa kwa akina Mama wajawazito wakati wa kujifungua lakini pia upasuaji wa kawaida kwa wagonjwa wengine watakaohitajika kupata huduma hiyo.

Naye ,Mganga mfawidhi wa Kituo cha Sabasaba, Dr. Henry Mungia, ameishukuru TAMISEMI kwa msaada huo huku akiahidi kuwa watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wagonjwa wa upasuaji wanapata huduma bora.

Dr. Mungia,amesema kuwa katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya katika Kituo chao cha Sabasaba, Kituo hicho kimetumi Milioni 54.7 kwa ajili ya kununua Ultrasound yenye thamani ya milioni 51 pamoja na Mashine ya kufulia nguo milioni 3.7.

Miongoni mwa Vifaa tiba  ambavyo Kituo kimepokea kutoka TAMISEMI ambavyo  vitatumika katika Chumba cha upasuaji ni Sterilization kwa ajili ya kuoeshea vifaa vya upasuaji, Kitanda cha wagonjwa wa upasuaji  Mashine ya kufulia, Taa za chumba cha upasuaji zinazosaidia kuona vizuri na kuzuia wadudu kupita wakati wa upasuaji, U.A.V kifaa kinachotumika kumuongoza Mtaalamu wa usingizi kipindi cha upasuaji, Saction Mashine inayotumika kusaidia kuvuta damu iliyo nyingi kwa mgonjwa na kuzuia mgonjwa aliye lazwa damu isiingie katika koo la hewa, Kitanda cha kusafirishia wagonjwa wodini kwenda chumba cha upasuaji , Oxygen Cylindre kinachotumika kuhifadhi gesi  pamoja na Ultra Sound ambayo Kituo imenunua kwa ajili ya kutumika kufuatilia maendeleo ya mama wajawazito na kuwa chanzo cha mapato kwa wagonjwa wengine.


JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.chombohurumedia .blogspot.com ku-install App ya chombohurumedia,  bila ya kuingia website

Tweet@chombo huru media,Youtube@chombo huru media, Facebook@chombo huru media, Instagram @chombohuru­­_media

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.