Header Ads

OCD MUJUMBA AFUNGUA MAFUNZO YA UDEREVA WA WAENDESHA PIKIPIKI ,BAJAJI NA GARI NDOGO KATA YA LUKOBE MANISPAA YA MOROGORO.

MKUU wa Polisi Wilaya ya  Morogoro OCD Dennis Mujumba, amefungua mafunzo ya Udereva wa waendesha Pikipiki, Bajaji, na magari madogo Kata ya Lukobe.

Mafunzo hayo yamefanyika Septemba 25/2023 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya St. Denis iliyopo Kata ya Lukobe.

OCD Mujumba, amesema dhumuni la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo madereva wawapo barabarani ili kuepusha  ajali.

"Dhana ya Polisi Jamii ni kuendelea kutoa elimu ili kupunguza uhalifu na wahalifu, lakini mafunzo haya ambayo wameyapata  tunaamini sasa madereva hawa  watakwenda kuepusha  ajali barabarani na watazingatia sheria za barabara" Amesema OCD Mujumba.

Aidha, OCD Mujumba, amesema mafunzo hayo yatasaidia sana madereva kuwa makini barabarani na kuwa mfano bora ili kujitofautisha na wasio na elimu ya udereva.

"Nimpongeze dada yangu Zuena Mwita huyu ni mpambanaji, nimeona jinsi anavyoishirikisha jamii hususani katika mambo mbalimbali  kama vile michezo kwa kuwa na ligi ya Pilisi Jamii, lakini na hili la mafunzo ni jambo zuri na la kuigwa, nitoe wito kwa madareva ambao hawajapata elimu warudi darasani wajifunze sheria za barabarani na jamii kwa ujumla niombe ili tuwe salama tufuate sheria na kujiepusha na vitendo visivyofaa " Amesema OCD Mujumba.

Hata hivyo amitaka jamii kufanya mambo ya kuigwa kwa kutumia miradi kama vile Familia yangu haina uhalifu, uzalendo, kupinga vitendo vya ubakaji na ulawiti, usalama wetu kwanza, utii wa sheria bila shuruti, urejeshwaji watoto mashuleni na uimarishaji vikundi vya ulinzi shirikishi.

 Diwani wa Kata ya Lukobe, Mhe. Selestine Mbilinyi, amewataka madereva hao ambao wamepatiwa mafunzo  kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha  ajali ambazo zimekuwa zikiacha majereha makubwa kwa familia ,kupoteeza nguvu kazi za Taifa na kuongeza tegemezi katika familia.

Naye Mkuu wa Kituo cha Polisi Kata ya Lukobe, Inspekta Zuena Mwita ambaye ndiye muandaaji wa mafunzo hayo , amebainisha kuwa mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi na weledi madereva ambao utapelekea kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Mwita,amesema lengo lake ni kuona Madereva wanafuata sheria za barabarani na kuendesha gari au vyombo vyao vya moto kwa mwendo ambao unatakiwa ili kuepusha ajali na kuokoa maisha ya wananchi.

Kwa upande wa madereva hao wamelishukuru Jeshi la Polisi hususani Polisi Kata wao kwa kubuni mafunzo hayo kwa sababu yanawakumbusha kufauata sheria za barabarani kutokana na wengi wanafanya kazi hiyo kwa mazoea.

Madereva hao  wameomba elimu hiyo na mafunzo hayo yawe endelevu kwa manufaa yao na kwa manufaa ya watumiaji wa barabara, wao wapo tayari muda wowote na pia wataendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.

Miongoni mwa wageni walioshiriki katika mafunzo hayo ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro OCD Dennis Mujumba, Diwani wa Kata ya Lukobe Mhe. Selestine Mbilinyi, Mtendaji wa Kata ya Lukobe, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Kata ya Lukobe pamoja na Afisa habari Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro .

Kauli mbiu ya Polisi Jamii "Polisi Jamii kwa Usalama na Maendeleo yetu" 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.