Header Ads

Bajeti ya Serikali 2022/2023 yatekelezwa kwa 96%.


WATENDAJI wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wamepongezwa kwa utendaji mzuri katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ambayo imetekelezwa kwa asilimia 96.

Pongezi hizo zimetolewa Septemba 07 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mhe. Jabir Makame kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-Maamry Mwamba wakati akifunga kikao kazi cha siku tatu cha tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya 2022/2023 na maandalizi ya bajeti ya 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa NSSF uliopo Manispaa ya Morogoro.


DC Makame ,amesema ushirikiano katika kutekeleza bajeti hiyo umewezesha kupata mafanikio katika utekelezaji wa shughuli za Serikali ambapo kwa asilimia 96 shughuli hizo zimefanikiwa hivyo amewashukuru na kuwapongeza kwa ushirikiano na utendaji kazi mzuri.

“...nitumie fursa hii kuwashukuru kwa ushirikiano na utendaji kazi mzuri katika utekelezaji mzuri wa bajeti ya 2022/2023 uliotuwezesha kupata mafanikio ambapo kwa asimilia 96 tumefanikiwa...”Amesema DC Makame.

Aidha, amesema kuwa Serikali itayafanyia kazi maoni yaliyotolewa na washiriki wa kikao hicho kwa kuwa wao ndiyo watekelezaji wakubwa wa bajeti katika maeneo yao.

Sambamba na hilo Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame amesema Serikali imezipokea changamoto zilizoibuliwa na wajumbe wa kikao hicho hususan katika uandaaji wa bajeti na kuahidi kuzifanyia kazi ili kuboresha utekelezaji wa bajeti hiyo.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Mipango na Uratibu Bw. Anza-Ameni Ndosa amesema kikao hicho kimelenga kujadili changamoto mbalimbali za utekelezaji wa bajeti na namna ya kutatua changamoto hizo.

Naye, Bw. Edson Toto ambaye ni Mchumi kutoka Wizara ya Fedha amesema kikao hicho kimehusisha washiriki kutoka Mikoa 13 ambapo Maafisa Mipango wa Mikoa na Halmashauri, Maafisa Rasilimali watu na Wahasibu ni walengwa wa kikao.

Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki  wa kikao hicho Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Mipango na Uratibu wa Mkoa wa Njombe Bw. Edward Mwakipesile ameshukuru na kuahidi kuyafanyia kazi  maelekezo waliyoyapata kwenye mafunzo ili kupata mafanikio chanya katika utekelezaji wa shughuli za Serikali katika maeneo yao.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.