Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA AFYA MAZINGIRA DUNIANI NA KUITAKA JAMII KUSHIRIKI KATIKA USAFI WA MAZINGIRA

MANISPAA ya Morogoro imeadhimisha Maadhimisho ya Siku ya Afya Mazingira Duniani kwa kutoa elimu katika maeneo ya migahawa, wauza vyakula mbalimbali.

Maadhimsiho hayo yamefanyika Septemba 26/2023 katika eneo la Stendi ya Mabasi Msamvu kwani eneo hilo limekuwa likichukua watu wengi ambao ni wasafiri .

Akizungumza juu ya maadhimisho hayo, Afisa Afya Manispaa ya Morogoro, Ndimile Kilatu, amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuhimiza ushiriki wa jamii katika uimarishaji wa huduma za afya mazingira.

Kilatu amesema kuwa asilimia kubwa ya magonjwa mengi yanayoathiri afya ya jamii yanatokana na uduni na uchafuzi wa mazingira na tabia hasi za kiafya.

Aidha, Kilatu amesema maadhimisho haya yanakuja kipindi ambacho nchi yetu ipo kwenye tahadhari ya kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na maafa yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa au mafuriko.

Hata hivyo,  amesema ili kusaidia kuepuka au kupunguza madhara ya kiafya yanayoweza kuletwa na mvua kubwa au mafuriko, lazima wananchi wachukue tahadhari kama vile kusafisha mitaro ya maji ya mvua ili kuzuia yasituame na badala yake kuruhusu maji kupita na kuenda sehemu husika, kusafisha maeneo yanayuzunguka ikiwa ni pamoja na kuondoa taka,kufunga matenki  ya kuhifadhia maji ili yasiingie takataka, kutumia choo bora kujisaidia  na kutotupa vinyesi vya watoto chooni.

Kwa upande wa Afisa  kutoka Ofisi  ya afya Manispaa ya Morogoro , Martin Mzuanda,amewataka wananchi kuzingatia kanuni za usafi wakati wote  ili kuepuka uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Afya Mazingira mwaka 2023 " Afya mazingira kwa dunia nzima ,shiriki kulinda afya ya kila mtu wakati wote".

Katika hatua nyengine, mratibu wa Chanjo Manispaa ya Morogoro , Philipo Bwisso, amesema Manispaa inaendelea na kampeni ya utoaji wa chanjo ambayo  imeanza Septemba 26/2023 hadi Septemba 30/2023.

Bwisso,  amesema, chanjo huokoa maisha ya mama na mtoto kwa kumkinga dhidi ya maradhi ambayo yanazuilika, na kuongeza kuwa kupata chanjo ni jambo la lazima kwavile inalinda pia kizazi kijacho dhidi ya magonjwa mbalimbali kama Surua na Polio.

Ni wajibu na jukumu la kila Mzazi kuhakikisha mtoto wake anapata chanjo kwani ni muhimu kwa afya na inazuia watoto kupata ugonjwa wa kupooza, wakina mama hakikisheni mnapata  chanjo zote kipindi cha ujauzito na wanapojifungua na kuhakikisha mtoto aliyezaliwa anapatiwa chanjo zote za utotoni ili kumlinda na maradhi kwani chanjo hizi ni salama na hazina madhara yoyote Kiafya”Amesema Bwisso.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.