WEZESHA MABADILIKO KUSAIDIA WAZEE 206 BIMA ZA AFYA KATA YA UWANJA WA TAIFA
TAASISI isiyo ya Kiserikali ya Wezesha Mabadiliko , imeahidi kuwasaidia jumla ya wazee 206 Kata ya Uwanja wa Taifa Manispaa ya Morogoro kupata Bima ya Afya iliyoboreshwa CHIF
Kauli hiyo ameitoa Mkurugenzi wa WEZESHA MABADILIKO Dkt. Lusako Mwakiluma akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Kata ya Uwanja wa Taifa yaliyofanyika Septemba 20/2023.
Aidha, Dkt. Lusako, amesema jukumu la kuwatunza na kuboresha maisha ya wazee pamoja na watu wenye mahitaji maalum, lisiachwe mikononi mwa Serikali na Taasisi binafsi bali kila mtu atambue anao wajibu wa kulitazama na kulitunza kundi hilo muhimu kwa ustawi wa Taifa.
‘’Wazee ni tunu ya Taifa na ndiyo waliotufikisha hapa tulipo hivyo ni jukumu la kila mmoja kuguswa na uwepo wa kundi hilo bila kusukumwa katika kutoa huduma hitajika na kuwafanya waendelee kufurahia uwepo wao’’Amesema Dkt. Lusako.
‘’Tumedodosa masuala mbalimbali ikiwemo Usalama, hitaji la chakula, mavazi, usafi, nk, lakini tumeona kipaumbele ni suala la Afya, wazee wengi wanashindwa kumudu gharama za matibabu’’Ameongeza Dkt. Lusako.
Kwa upande wa Mratibu wa Wazee Manispaa ya Morogoro, Hamisa Kagambo, ameishukuru Taasisi ya WEZESHA MABADILIKO na kutoa wito kwa Taasisi nyingine za Kiraia kusaidia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kundi hilo.
‘’Awali nitoe Shukurani kwa Taasisi ya WEZESHA MABADILIKO ( WEMA ) , lakini niziombe Taasisis nyingine katika Manispaa yetu ya Morogoro kusaidida katika kukabili changamoto zinazowakabili wazee wetu Manispaa ya Morogoro ili waweze kuishi kwa furaha na amani’’ Amesisistiza Kagambo.
Naye Diwani wa Kata ya Uwanja wa Taifa , Mhe. Rashid Matesa, amesema WEZESHA MABADILIKO wamekuwa na mchangi mkubwa katika Kata yao kwani sio afya tu wamekuwa wakijitoa katika mahitaji mbalimbali .
Matesa, amesema kwa kushirikiana na Ofisi yake ya Kata watahakikisha wazee wanaendelea kupata huduma bora na wanapewa vipaumbele katika vituo vya huduma za afya.
Baadhi ya wazee walioshiriki katika maadhimisho hayo hawakusita kutoa Shukurani zao huku wakiiomba Serikali, Wadau pamoja na Jamii kwa ujumla kutowasahau huku wakisisitiza kuwa wao ndio waasisi wa Taifa na Maendeleo yaliyopo leo wamehusika kwa kiasi kikubwa kuhakikisha yanafikiwa.
Post a Comment