Header Ads

Mashirika yasiyo ya Kiserikali yatakiwa kupanua wigo wa huduma kwenye maeneo yenye uhitaji.



MASHIRIKA  yasiyo ya Kiserikali Mkoani Morogoro yametakiwa kupanua wigo wa utoaji huduma kwenye jamii katika maeneo ambayo hayajafikiwa ili kutoa fursa ya sawa kwa huduma zinazotolewa.

Hayo yamesemwa Septemba 07/2023  na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima  wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashirika hayo yaliyopo Mkoani Morogoro uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

DC Makame amesema baadhi ya mashirika hayo hutekeleza shughuli zake kwa kuchagua maeneo hususan maeneo ya mijini hivyo kupunguza fursa kwa maeneo mengine kupata huduma zinazotolewa na mashirika hayo, hivyo ameyataka mashirika hayo kuyafikia maeneo ambayo yanauhitaji hususan maeneo yaliyo pembezoni mwa mji.

“...naomba nitoe msisitizo kwamba katika kutekeleza majukumu yenu ni vyema pia kuangalia maeneo ambayo yanauhitaji vile vile ikiwemo katika Wilaya zingine za pembezoni...utakuta mashirika mengi yapo mjini...” Amesema DC Makame.

Aidha, amesema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inatambua mchango wa Mashirika hayo katika kuleta maendeleo kwenye sekta mbalimbali za Afya, elimu, maji, mazingira, kilimo, upingaji wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na uimarishaji wa uchumi wa kaya.

Sambamba na hilo, DC Makame, ameyataka mashirika hayo kutojikita katika miradi ambayo ni kinyume na mila, tamaduni na maadili ya Watanzania na kwamba Serikali haitashindwa kuyachukulia hatua mashirika yatakayo jihusisha na ukiukaji wa tamaduni za watanzania.

Kwa upande wao wadau wa Mashirika hayo Mkoani humo akiwemo Mjumbe wa Uratibu kutoka Taasisi ya Acts of Life Dkt. Francis Nyakamwe amebainisha changamoto zinazoyakabili mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoani humo zikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha, sheria kandamizi zinazowabana katika utendaji kazi zao, wingi wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo hawana uelewa nazo.

Aidha, wadau hao wamependekeza kuwepo kwa miongozo ya moja kwa moja ya usajili hii ni kutokana na changamoto ya mashirika hayo kutakiwa kusajiliwa kwa mara ya pili hususani kwenye maeneo wanayokwenda kutekeleza shughuli zao.

Kikao hicho kimelenga kujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto zinazoyakabili mashirika hayo pamoja na Serikali kutoa maelekezo kwa mujibu wa sheria, kanuni na sera zinazotolewa mara kwa mara.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.