MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA USAFISHAJI DUNIANI KWA KUSHIRIKI NA WADAU WA MAZINGIRA KUFANYA USAFI ENEO LA MSAMVU.
MANISPAA ya Morogoro, kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wa Mazingira wameadhimisha siku ya Usafishaji Duniani kwa kufanya usafi katika eneo linalozunguka Stendi ya Mabasi Msamvu ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha Jamii kujenga tabia ya usafi katika maeneo wanayoishi na wanayofanyia shughuli zao mbalimbali.
Akiongea kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ,Salome Magembe ambaye ni Afisa Lishe Mkoa wa Morogoro amesema ujumbe wa Mwaka huu ni “Kujifunza kupanga na Kuhimiza Uimarishaji Huduma za Udhibiti wa Taka" hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anatunza mazingira yanayomzunguka iwe ni nyumbani ama katika biashara.
Magembe,amesema wapo watu ambao hawafanyi usafi mpaka kusimamiwa na kuonya kuwa wahakikishe wanatii sheria bila shuruti kwani suala la uchafuzi wa Mazingira halina msamaha.
“Uchafu unaozalishwa na mtu mmoja huathiri watu zaidi ya mia moja kwani huweza kusababisha mlipuko wa magonjwa”Amesema Magembe.
Naye Afisa Tarafa Manispaa ya Morogoro, Winfred Kipako, amewataka wananchi, wdau wa Mazingira itumie siku hiyo ikiwa ni njia moja wapo ya kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya usafi kwa kupenda mazingira yaliyo safi kwa usalama kwa afya zao.
Diwani wa Kata ya Mafisa, Mhe. Joel Kisome, amesema usafi ni jambo la lazima hivyo wale ambao watakwenda kinyume na Serikali na kuwa wachafuzi wa Mazingira watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wa Afisa Afya Manispaa ya Morogoro, Ndimile Kilatu, amesema zoezi hilo la usafi kwa Manispaa ya Morogoro linapaswa kufanyika kwa nguvu zote huku akiwataka na wananchi kuhakikisha wanalipa ada ya tozo za usafi wa kila mwezi ili kuendelea kuweka Mji safi.
Kilatu, amewataka Mama lishe, mafanyabiashara wote wenye fremu na vibanda pamoja na wamiliki na madereva wa mabasi ya usafirishaji kuhakikisha katika maeneo yao wanaweka dastibi za kuhifadhia taka na watakao kiuka watatozwa faini na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kaimu Mganga Mkuu Manispaa ya Morogoro, Dr. Angela Kalimenze, amewashukuru wananchi ,Viongozi na wadau wa mazingira na wanafunzi wote waliojitokeza katika maadhimisho hayo ya usafishaji.
Manispaa ya Morogoro hufanya shughuli ya usafi kila mwisho wa wiki (Jumamosi) ambapo wananchi katika makazi yao na maeneo ya biashara huwajibika kufanya usafi.
Tweet@chombo huru media,Youtube@chombo huru media, Facebook@chombo huru media, Instagram @chombohuru_media
Post a Comment