WATUMISHI WASHAURIWA KUFANYA MAANDALIZI YA KUSTAAFU WANAPOANZA KUAJIRIWA.
WATUMISHI nchini wameshauriwa kuanza kufanya maandalizi ya kustaafu kipindi wanapoanza ajira zao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu ,Mahakama ya Tanzania, Edward Nkembo, leo Julai 26/2021 kwenye Ukumbi wa Magadu uliopo Manispaa ya Morogoro wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Watumishi wa Mahakama wanaojiandaa kustaafu.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Nkembo, amesema suala la maandalizi ya kustaafu ni muda wowote ambapo mtumishi ameanza kuajiriwa.
Nkembo, amesema kuna aina mbalimbali za kustaafu ikiwamo kufukuzwa, kuacha kazi, kufariki pamoja na umri wa kisheria wa miaka 55-60.
Amesema kuwa uchunguzi pamoja na uzoefu wa miaka mingi hapa nchini unaonyesha watumishi wengi wameshindwa kujiandaa vema na maisha baada ya kustaafu kutokana na kipato kidogo muda wote wa ajira na hivyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali wakati wa kustaafu.
Amesema changamoto zinazowakabili watumishi baada ya kustafu ni pamoja na kushindwa kupata mahitaji ya lazima kama chakula na mavazi, kukosa kipato cha kusaidia familia zao, wengine kuoa na kutapeliwa mafao yao, kubadili tabia na kuanza kuishi maisha ya starehe, kuanzisha miradi mipya ambayo hawakuwahi kuijua, kupokea ushauri kuhusu shughuli ya kufanya kutoka kwa watu mbalimbali, kugawa mafao kwa watoto na watu wengine, kuanza miradi mikubwa ya ujenzi, kufilisika ndani ya muda mfupi sana na kufariki kutokana na ugumu wa maisha katika muda mfupi sana.
"Ndugu washiriki nimeona changamoto hizi niziweke kwenye ratiba yenu ya mafunzo ikiwa ni pamoja na matumizi ya muda, kupanga kustaafu, mipango binafsi ya fedha, fursa na changamoto za kustaafu, ujasiriamali, uwekezaji, mambo ya afya na mengine, hivyo matumaini yangu mtatumia fursa zote kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ambayo mnaweza kuanza kuyafanya sasa na kuendelea nayo mara baada ya kustaafu kwa faida zenu na kwa familia zenu kwa ujumla" Amesema Nkembo.
Kwa upande wa mratibu wa mafunzo mafunzo hayo, Bw. Nuhu Mtekele, amewata watumishi kusikiliza kwa makini mafunzo hayo kwani yamejaa ujuzi mkubwa wa kuweza kukabiliana na changamoto mara baada ya kustaafu.
Mtekele, amesema wakati watumishi wakitafuta namna bora ya kutumia fedha hizo , wapo watu wanaopanga namna yakuzipata fedha hizo walizokusanya kwa kipindi chote wawapo katika ajira.
Amesema miongoni mwa namna ya watu wanaotafuta mbinu ya kutumia fedha za wastaafu ni pamoja na wizi wa mitandao, utapeli na rushwa ambayo ni matukio mabaya ambayo wastaafu wengi wamejikuta wakiwa ni wahanga wa matukio hayo.
" Nitoe rai kwenu kutambua uwepo wa matukio hayo niliyoyataja na kuchukua tahadhari zote za kukabiliana nazo, matumaini yangu kuwa mafunzo haya kwa ujumla yatawasaidia kuweka mikakati ya namna ya kufanya shughuli halali za ujasiriamali na kijamii kwa maendeleo yenu wenyewe na jamii kwa ujumla na kuwasaidia kujua namna bora ya matumizi ya mafao yenu mara baada ya kustaafu" Amesema Mtekele.
Post a Comment