Header Ads

MAMIA YA WANANCHI WAFURIKA MAPOKEZI YA RAIS SAMIA MANISPAA YA MOROGORO , ATOA NENO KUHUSU KULINDA AMANI




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimia na Wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
Mamia ya wananchi waliojitokeza katika mapokezi ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Stendi ya Mabasi Msamvu.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kuendelea kulinda amani na umoja kwa ajili ya kujenga Taifa.

Kauli hiyo, ameitoa Julai 8/2021 , wakati akizungumza na wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro katika eneo la Stendi ya Mabasi Msamvu.

Mhe. Samia, amesema wapo watu wanaleta vurugu jambo ambalo halina afya kwa kwa nchi hii na kusababisha kuchelewa kupata maendeleo.

Aidha, amesema changamoto zote zikiwemo za ardhi, biashara , elimu, maji na miundombinu Serikali ipo makini na tayari hatua zimeshachukuliwa ili wananchi waendelee kupata huduma bora.

Amesema kuwa Serikali itahakikisha kuwa inatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM kwa vitendo ili yale yote yaliodhamiriwa kufanyika yanafanyika na kuleta matunda .

"Serikali tunatekeleza Ilani ya CCM kwa asilimia kubwa, tuna miradi mikubwa tumeshaanza kuitekeleza na inaendelea vizuri,  tayari huduma za afya, maji , miundombinu tumeshaanza kuboresha kwa asilimia kubwa, niwaombe sana Viongozi mliopewa dhamana fanyeni kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi ambao wanamatumaini makubwa na Serikali yao, imarisheni ulinzi na usalama ili Taifa letu liendelee kuwa nuru kubwa ya amani Afrika nzima na Duniani Kote, Taifa likiingia katika machafuko hata hayo maendeleo tunayoyataka sasa hatutayapata tena" Amesema Samia.

"Leo nimepita kuwasalimia, kuonana na kutambuana, sio ziara yangu rasmi ya kikazi, kama  Mkuu wa Mkoa alivyoniomba kuja kufanya ziara , niwaahidi nitarudi kufanya ziara Mkoa huu ili tuzungumze kwa pamoja na tuone jinsi gani tunavyoweza kushirikiana kusongesha Taifa mbele kimaendeleo" Ameongeza Mhe. Samia.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela, amempongeza Rais Samia, kwa kuipatia Mkoa wa Morogoro miradi mikubwa ya Kimkakati.

Shigela, amesema kwa kushirikiana na Viongozi wa Mkoa wa Morogoro watahakikisha miradi hiyo ya kimkakati inafanya kazi na kuendelea kuwahudumia wananchi.

"Tunashukuru sana kwa ujio wako Mhe. Rais, wana Morogoro wanaimani kubwa sana na wewe , tunaomba ufike kufanya Ziara ili wananchi hawa wakusikie na kupokea maagizo yako, Manispaa yetu ya Morogoro tunatamani siku Moja iwe Jiji, lakini tunaamini hilo linawezekana kama tukiendelea kujipanga vizuri na kila mtu akafanya kazi kwa nafasi yake " Amesema Shigela.

Katika hatua nyengine, amempongeza sana Rais Samia kwa kukutana na Wananchi wa Manispaa ya Morogoro na kumuomba kutenga muda wa kufanya ziara katika Mkoa wa Morogoro ambapo Rais Samia amekubali ombi hilo.

Kwa upande wa Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Fikiri Juma, amemuomba Mhe. Rais kusaidia kuweza kufufua Viwanda vilivyokufa Manispaa ya Morogoro kwani asilimia kubwa ya Viwanda hivyo vilikuwa vinatoa ajira kwa wananchi.

Fikiri, amesema asilimia kubwa ya Wananchi wa Mkoa wa Morogoro ajira kubwa wanategemea Viwanda katika kuendesha Maisha yao.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.