Header Ads

Waratibu wa CHF watakiwa kusimamia makusanyo ya fedha za wanachama wake.

 


Waratibu wa Mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF) Mkoa wa Morogoro wametakiwa kusimamia makusanyo ya fedha za wananchama wa Mfuko huo pamoja na kufuatilia huduma za Afya zinazotolewa kwa wananchi wake ili kutoharibu taswira njema ya Serikali kuhusu mpango na lengo la CHF.

Agizo hilo limetolewa Julai 2, mwaka huu na Katibu Tawala Msaidizi Upande wa Serikali za Mitaa Bw. Leopold Ngirwa wakati akifungua kikao kazi cha watendaji wa iCHF iliyoboreshwa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro. 

Bw. Leopold Ngirwa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja amewataka Waratibu hao kusimamia kwa umakini shughuli za uandikishaji na ukusanyaji wa mapato ya fedha za wanachama wa iCHF na kuhakikisha fedha hizo zinaingizwa katika akaunti ya Mkoa kwa wakati.


“Kasimamieni kwa umakini shughuli za uandikishaji na makusanyo ya fedha za wanachama wa iCHF na kuhakikisha fedha zinaingizwa katika akaunti ya Mkoa kwa wakati” amesema Leopold Ngirwa. 

Katika hatua nyingine Bw. Ngirwa amewataka waratibu kwa kushirikiana na Wanganga Wakuu wa Wilaya Mkoani humo kufuatilia kwa karibu huduma za Afya zinazotolewa kwa wananchama wa CHF endapo wanapata huduma inayostahili ili kutoharibu taswira na lengo la mfuko huo.lengo la Mkoa huo ni kuona kila mwananchi aliyejisajiri kwa shilingi elfu Thelathini katika Mfuko wa Bima ya Afya anapata huduma ya matibabu bure kwa kipindi cha mwaka mzima.

Awali akiwasilisha ripoti ya Mkoa huo Mratibu wa iCHF Mkoa wa Morogoro Bi. Elisia Mtesigwa amesema bado wanaendelea na uhamasishaji ili kuyafikia makundi mbalimbali ndani ya jamii kujiunga na mfuko wa iCHF, huku akieleza lengo lake sio  kuwa na wanachma wengi bali kuhakikisha kila mwananchi Mkoani humo anakuwa na uhakika wa kupata matibabu ya Afya yake wakati wote hata anapokuwa hana fedha mkononi. 

Aidha, Bi Elisia amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hawakufikia malengo ya uandikishaji kwa wanachama waliolengwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa fedha za uandikishaji kwa ajili ya kufanya uhamasishaji wa uandikishaji kwa wanachama.

Sambamba na sababu hiyo, amebanisha kuwa bado kuna changamoto chache  zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji hafifu wa shughuli za mfuko huo na baadhi ya Halmashauri kutowasilisha taarifa ya utendaji wa kila msimamizi katika vikao vya tathimini.

Naye Elizeus Rwezaula, kutoka mradi wa Tuimarishe Afya – HPSS aliyeshiriki kikao kazi hicho, amebainisha mafanikio ya mfuko huo tangu kuanzishwa kwake ambapo amesema hadi kufikia Juni mwaka huu asilimia 6 ya wananchi kote nchini wamejiunga na mfuko huo na wanaweza kupata huduma za matibabu katika vituo vyote vya Afya vilivyopo hapa nchini.

Nao washiriki wa kikao kazi hicho akiwemo Mwaisongo Raphael ambaye ni Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba amewataka wananchi kujiunga na Bima ya CHF kwa kuwa inawawezesha kupata huduma ya Afya kwa bei nafuu kwa kulipa elfu thelathini tu kwa watu sita na kupata huduma ya Afya kwa kwa mwaka mzima.

Aidha, ametaja uelewa mdogo wa wananchi wengi kuwa ni changamoto ndani ya mfuko huo, kwani wengi wanapokwenda kupata huduma ya Afya na kukosa aina moja ya dawa inakuwa kero kubwa bila kuangaliwa faida nyingine wanazopata kama ya kutibiwa kwa mwaka mzima kwa Sh. Elfu thelathini na kupata huduma ya vipimo ukilinganisha na kama angejighalimia.

Kwa sababu hiyo Bw. Mwaisongo ameiomba Serikali kuongeza zaidi upatikanaji wa dawa kwa ajili ya wanachama wake wa Mfuko huo ili wengi wavutike na hivyo kuokoa maisha yao kwani hakuna jambo muhimu katika maisha zaidi ya kuwa na Afya Bora

Zaidi ya wanachama 56, 000 Mkoani Morogoro wamejiandikisha katika mfuko wa Bima ya Afya iliyoboresha – iCHF kwa mwaka wa fedha 2020/2021 sawa na asilimia 9.5 ya kaya 590,006 ambapo kaya 21, 941 kati ya hizo zinaweza kupata matibabu katika vituo vya kutolea huduma za Afya. 

Mpango wa Bima ya Afya ya iCHF ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Serikali iliyopo madarakani. Ibara ya 83 (e) ukurasa wa 186 kuimarisha mifuko ya Bima za Afya nchini ikiwemo mifuko ya Bima za Afya ya (NHIF na CHF) ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na Bima ya Afya kwa wananchi wote.



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.