Header Ads

DIWANI Mafiga ageuka mbogo suala la uchelewaji Kazini.

Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile (kushoto)  akiongozana na Mkuu wa Shule ya Sekondari Mafiga wakati wa ziara ya kukagua shule hiyo.

DIWANI wa Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro, Mhe. Thomas Butabile, amegeuka mbogo baada ya kukuta baadhi ya watumishi wakiwa wamechelwa kufika Ofisini kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Hayo yamejiri leo Julai 19/2021 alipokuwa katika ziara fupi ya kufuatilia suala la nidhamu kazini ya kujali muda wa kuwahi kazini kwa Watendaji na Watumishi katika Kata ya Mafiga.

Akizungumza hayo mapema Mhe. Butabile,  amesema bado wapo watumishi wamekuwa na nidhamu mbovu ya kuchelewa kazini jambo ambalo limekuwa sugu huku akiwataka watumishi kubadilika na kuendana na kasi ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya Kazi iendelee.


"Mpo hapa kwa ajili ya kumsaidia Mhe. Rais , Samia Suluhu Hassan, hivyo wafanyakazi mnawajibu wa kuwahi kazini saa 1:30 asubuhi kama ilivyopangwa kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Umma na kutoka saa 9:30 Mchana baada ya muda wa kazi, hatuwezi kuendelea kuvumilia tabia ya watu kuendelea kumwibia Mwajiri muda wa kufanya kazi,hatuwezi kuleana ndio maana tuliomba nafasi hii ya kusimamia maendeleo ya Kata tukiwa na lengo kuwa lazima maendeleo yaonekane na wananchi wanufaike na matunda ya viongozi wao , tusifanye kazi kwa mazoea lazima tujitambua na tuone sisi tuna nafasi gani kwa jamii " Amesema Mhe. Butabile.

Aidha amewaagiza wakuu wa taasisi hizo ikiwemo Vituo vya afya pamoja na Shule wachore  mstari mwisho katika daftari  la mahudhurio kwa peni nyekundu ili watakaochelewa wachukuliwe hatua za kisheria .

Amesema kuwa  suala la kuchelewa kazini bila taarifa ya msingi  ni  utovu wa nidhamu jambo linalosababisha kuchelewa  kupata huduma na  kuchelewesha maendeleo.

"Leo nimeona nifanye ziara hii fupi ya kushtukiza kwa kupitia katika Kata yangu ili kuangalia mahudhurio ya watumishi , lakini nilichobaini bado kuna hali ya nidhamu mbovu ya kuchelewa kazini, katika tembea yangu baadhi ya shule nimemkuta waalimu wengi wanachelewa shule, wengine walinifuata kuomba msamaha kiukweli kwa hili  sijafurahishwa na hali hii, huku ni kuwaibia Wananchi pesa zao , wanyonge wamekuwa wakilipa pesa nyie mnalipwa mishahara tuache mara moja tabia hii turudi katika nidhamu ya kuwahi na kutoa huduma, nyie mnapewa misharahara hamuitumii ipasavyo maana usipokuja na ukija bado mishahara yenu ipo pale pale , tubadilike tufanye kazi na mishahara yetu ni nguvu za wanyonge amabo tuna wajibu wa kuwatimizia kero zao na kutoa huduma nzuri bila ya upendeleo na hata shuleni tukiwahi mapema tutaweza kuchangia ongezeko la ufaulu kwa watoto wetu " Ameongeza Mhe. Butabile.


Hata hivyo, amesema kuwahi kazini kuna kwenda na kuanza kazi muda huo huo sio mtu anawahi kazini kisha anaanza  kusoma magazeti au kupiga soga kwa hili hata weza kulifumbia macho na atawachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa wale wenye tabia kama hizo.

Amesema katika Kata yeke  anataka kazi zifanyike na kama yupo mtumishi au mtendaji anaona hawezi kuendana na kasi yake atafute mahala pengine kwa kufanyia kazi na sio katika Kata ya Mafiga.


Mbali na Waalimu  pia amewataka watumishi wa ngazi ya Huduma ya afya na Ofisi ya Kata  kuzingatia muda wa kuingia kazini na kuwatumikia wananchi ili kero zote zilizopo mitaa zipungue na kuepusha mabango yanayoandaliwa na Wananchi kufuatia ujio wa Viongozi wa Juu wa Nchi wanapofanya ziara.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.