MHE. MABULA APIGA MARUFUKU UJENZI WA MAENEO YA WAZI YA SERIKALI.
NAIBU Waziri wa ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Angeline Mabula, amepiga marufuku ujenzi katika maeneo ya wazi yote huku akiwatahadharisha wanaofanya hivyo.
Kauli hiyo ameitoa Julai 13/2021kwenye eneo la Stendi ya Daladala Mafiga Manispaa ya Morogoro wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku 2 ya kusikiliza na kutataua kero za migogoro ya ardhi Mkoa wa Morogoro.
Kauli ya waziri imekuja kutokana na kukithiri kwa watu kufanya ujenzi maeneo ya wazi na wamekuwa wakidai kuwa na vibali vya Manispaa.
Akiziungumza na wananchi waliojitokeza katika mkutano huo wa hadhara, Mhe. Mabula,amesema kuwa kumeibuka wimbi la wananchi ambao wamekuwa wakienda kinyume na sheria za mipango miji ya kujenga nyumba katika maeneo ya wazi.
Mhe. Mabula ,amesema kuwa sheria itachukua mkondo wake dhidi ya wote ambao watakaidi na kufanya ujenzi kwenye maeneo hayo.
"Lengo la kuja hapa kuongea na nyinyi leo ni kusikiliza na kutatua kero za migogoro ya ardhi pamoja na kuangalia wale ambao wamekuwa wakijenga katika maeneo ya wazi ya Serikali, kumbukeni hayo maeneo ya wazi Serikali imeyatenga kwa kazi maalumu, sasa unapojenga hapo unajitafutia mgogoro ambapo mwisho wa siku huna chako, acheni mara moja hiyo tabia lengo la Serikali sio kumnyanyasa mwananchi lazima muyaheshimu hayo maeneo" Amesema Mhe. Mabula.
Aidha, amesema migogoro mingi imekuwa ikisababishwa na viongozi kuanzia ngazi ya Vitongoji hadi Manispaa.
"Wapo viongozi wanaochukua maeneo ambapo wanasababisha changamoto zisizo na sababu, niwaombe watumishi wa Halmashauri zote nchini , popote nitakapo kuta kuna kesi ya kiongozi na mtu wa kawaid a na mtu wa kawaida umemkuta pale basi tutaomba hati hiyo ifutwe na kubadilishwa kwa sababu kesi zinakuwa ninyingi ukiangalia watumishi wamehusika na zaidi ni mtu mwenye madaraka , hatupingani na maamuzi ya Mahakama, tunachosema ni taratibu za utendaji kazi ndani ya Ofisi za Serikali,tusingependa kesi za namna hiyo zijirudie" Ameongeza Mhe. Mabula.
Katika hatua nyengine, amewaagiza Wakurugenzi wote nchini kwa kushirikiana na Watendaji ngazi ya Kata kuhakiksiha wanakuwa na majukumu ya kuangalia ujenzi holela unaofanywa katika maeneo yao na kuweza kudhibiti .
"Yoyote anayejenga katika eneo liwe limepimwa au halijapimwa akuonyeshe kibali, maeneo yote yameshatangazwa kuwa ni maeneo ya mji, haiwezekani mtu ajenge kama yupo kwnye kijiji , wakurugenzi mkikuta maeneo nyumba zimeshamiri bila mpangilio ,angalieni namna ya kuwashughulikia watendaji wenu wa Kata kwani ujenzi bila vibali ni chanzo cha ujenzi holela" Amesisitizia Mhe. Mabula.
Kwa upande wa Kamishina Msaidizi wa ardhi Mkoa wa Morogoro, Frank Minzikutwe, amesema ujenzi holela na uvamizi wa maeneo vimekuwa vyanzo vikubwa vya kuzalisha migogoro katika maeneo mengi jambo ambalo linapaswa ushirikiano mkubwa wa kuweza kudhibiti matukio kama hayo.
"Tutaanza kuwa wakali sana katika ujenzi holela, hali sio shwari kabisa, mnatudharirisha watendaji wenu tunaonekana hatufanyi kazi, mkianza kujenga kiholela hadi milimani unafikiri hata hayo maji tunayoyategema kutoka Mindu hatutayapata, uchafu kwenye bwawa hautapungua, niwasihi sana ndugu zangu acheni ujenzi holela na tutapita kuangalia maeneo hayo na wale wanaofanya hivyo tutachukua maamuzi magumu" Amesema Minzikutwe.
Aidha, Minzikutwe, ameelezea eneo la kichangani ambalo Serikali imelitenga huku akiwataka wananchi wanaofanya shughuli eneo hilo kutambua mali hiyo sio yao na wao walihifadhiwa mpaka Serikali itakapo taka kufanya matumizi yake.
" Eneo la Kichangani Manispaa ya Morogoro ni eneo la Serikali ambapo ilitenga kwa ajili ya matumizi ya kujenga Kituo cha kufanya ukarabati wa terni zetu, Serikali iliwachia wananchi wafanye shughuli zao ili waweze kujikimu , sasa wale wananchi kila siku wanaandamana wanasema sisi ndio tuliondoa mkonge , eneo hilo walipewa msaada wa kujikimu, sasa nimewaelekeza wenzetu wa Reli wasimamishe shughuli za kilimo katika hilo shamba ili kazi yao iwe ni kufyeka , kwani watu wakisaidiwa wanajiona kama ni wamiliki na , eneo hilo bado ni la Serikali na hatujapata maelekezo yoyote" Amesema Minzikutwe.
Post a Comment