Header Ads

KATIBU TAMISEMI AFANYA ZIARA MABWENI YALIYOUNGUA NA MOTO SHULE ZA SEKONDARI MANISPAA YA MOROGORO.

 

Katibu  Mkuu  Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akikagua Bweni la Wanafunzi wa Kidato cha kwanza liloungua moto katika  Shule ya Sekondari Charlotte.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando (kushoto) , Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro Pili Kitwana (katikati), OCD  Wilaya ya Morogoro, Georgina  Richard Matagi (kulia)wawakifuatilia janga la kuungua kwa moto mabweni ya Shule.

Kamanda wa ZimaMoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Goodluck Zelote (kulia), akifuatilia kwa makini janga la moto la Mabweni.

                                          

KATIBU  Mkuu  Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe, amefanya ziara ya kutembelea katika Mabweni yaliyoungua na moto shule za Sekondari mbili  ikiwemo shule ya Wasichana ya Kiislamu ya AT-TAAUN na Shule ya Sekondari Charlotte zilizopo Manispaa ya Morogoro.

Ziara hiyo imefanyika leo, Julai 11/ 2020 majira ya asubuhi ya saa 3 akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando, Kamati ya ulinzi na usalama  , Kamanda wa Jeshi la ZimaMoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro , Goodluck Zelote, pamoja na Uongozi wa Manispaa ya Morogoro ukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Pili Kitwana.

Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe, amesikitishwa na uharaibifu wa moto ulioteketeza mali za wanafunzi huku akiwataka waalimu, wanafunzi pamoja na Uongozi wa shule kuwa na subra katika kipindi hiki kifupi  cha mpito.

Prof. Shemdoe, amewaomba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zima moto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro washirikiane vyema katika kufanya kutathmini madhara yaliyojitokeza kutokana na moto huo ili Serikali iweze kuwa na taarifa kamili na kujua nini kinaweza kufanyika .

Mwisho, Prof. Shemdoe, amewataka wasimamizi wa Shule kuhakikisha wanafanya maboresho ya mifumo ya umeme mara kwa mara ili kuweza kuzuia majanga kama hayo kutokea.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando  kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Morogoro ,  amemshukuru Prof. Shemdoe kwa ziara yake ya kuwatia matumaini waalimu, wanafunzi pamoja na Uongozi wa Serikali.

DC Msando, amesema kuwa tayari wao kama Viongozi wa  Serikali mara baada ya kupata taarifa ya kuungua kwa mabweni , wamechukua  hatua ikiwemo ya kuhakikisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  linafika eneo husika na kufanikisha kuuzima moto huo katika shule hizo mbili.

"Tumeona madhara yaliyotokea  katika mabweni ya shule zetu, Jeshi la zimamoto limefanya kazi yake vizuri, nawapa pole sana, lakini kikubwa niwasisitize wasimamizi wa shule waendelee kuchukua tahadhari zote muhimu ili majanga kama haya yasijitokeze tena, naomba sana Uongozi wa Shule husika wawe na subra katika kipindi hiki cha uchunguzi naamini tukishajua chanzo ninini , basi tutawapa taarifa sahihi juu ya nini kinapaswa kufanyika" Amesema DC Msando. 

Kwa upande wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Charlotte , Sister Agness Wilson, amemshukuru Katibu wa TAMISEMI, Uongozi wa Mkoa , Wilaya na Manispaa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuwa karibu sana na matatizo yaliyowakumba huku akisema ujio wa viongozi hao umewatia moyo wa kuendelea kufanya kazi .

" Tunawapongeza sana Viongozi wetu , ujio wao umetupa nguvu na matumaini, ukiangalia hapa madhara makubwa ni kuungua kwa vitu , moto huu ulitokea Julai 10, majira ya saa 3 asubuhi lakini tunamshukuru Mungu aliweza kutuepusha na janga hilo, hakuna aliyefariki wala kujeruhiwa, zaidi tu ni kuungua kwa bweni la kidato cha kwanza wasichana ambapo tukio hilo linatokea wao walikuwa madarasani, tukawahamisha wote ambao wamekutwa na majanga kuwaweka katika mabweni ya wanafunzi wa Pre- Form 1, lakini sasa tunaendelea vizuri na wanafunzi wanasoma kama kawaidia licha ya matatizo hayo" Amesema Sister Agness.

Shule ambazo mabweni yao yamepatwa kuunguliwa kwa moto ni pamoja na shule ya Kiislamu ya  Wasichana ya AT-TAAUN iliyopo  Kata ya Mji Mpya  ambapo bweni la  ghorofa ya juu yenye vyumba 6 vya madarasa vinavyobeba jumla ya wanafunzi 120,  pamoja na Shule ya Sekondari Charlotte iliyopo Kata ya Tungi ambayo iemungua bweni moja la wanafunzi wa kidato cha kwanza upande wa wasichana.

Mpaka sasa jeshi la Polisi Wilaya ya Morogoro  kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogor  wapo katika hatua za kufanya tathmini juu ya madhara yaliyosababishwa na janga hilo kisha baada ya kupata taarifa itawasilisha katika mamlaka ya juu ili kuona nini kinapaswa kufanyika.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.