Header Ads

PROF. NOMBO AVITAKA VITUO VYA UFUNDI STADI KUPEWA VIPAUMBELE.


Naibu  Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,akizungumza na wanafuzni wa Kituo cha Ufundi Stadi Shule ya Msingi Msamvu 'A'.
Wanafunzi wa Kituo cha mafunzo ya Ufundi Stadi kilichopo Shule ya Msingi Msamvu 'A'.
Naibu  Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,akizungumza na Waalimu wa Shule ya Msingi Msamvu 'A', (kulia) Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro, Chausiku Masegenya.
Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro, Chausiku Masegenya.
Naibu  Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,akizungumza na Waalimu wa Shule ya Msingi Msamvu 'A', pamoja na waalimu wa Kituo cha Ufundi Stadi.
Naibu  Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,akiambatana na viongozi katika picha ya pamoja na Wanafunzi  wa Kituo cha mafunzo ya Ufundi Stadi kilichopo Shule ya Msingi Msamvu 'A'.
Waalimu wa Shule ya Msingi Msamvu 'A',

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amevitaka vituo vya mafunzo ya ufundi stadi pamoja na Vyuo vya Ufundi kupewa vipaumbele katika kuzalisha wataalamu.

Kauli hiyo, ameitoa Julai 15/2021 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Chuo cha VETA Morogoro pamoja na kituo cha mafunzo ya ufundi stadi kilichopo Shule ya Msingi Msamvu 'A' Manispaa ya Morogoro.

Akiziungumza na Waandishi wa habari, Prof. Nombo, amesema kuanzishwa vituo hivyo ni kuweza kuwasaidia Vijana katika kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.

Aidha, amewataka wasimamizi wa vituo hivyo vya ufundi stadi wakiwemo Wakurugenzi husika wa Halmashauri kuhakikisha wanafanyia kazi changamoto zinazojitokeza ikiwemo vyumba vya madarasa, vitendea kazi  na karakana ili kuwafanya Vijana kupata kile ambacho kinahitajika katika kuelekea uchumi wa viwanda.

"Kwa kuzingatia mkakati na mwelekeo wa nchi ambapo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan , amekuwa akihubiri sana suala la elimu ya ufundi stadi, amekuwa akiagiza kuwa waalimu waweze kuzalisha Vijana wenye ujuzi  mara wamalizapo shule, jambo ambalo litawapelekea  kujiongezea ujuzi na ubunifu utakaowawezesha kujiajiri" Amesema Prof. Nombo.

Amewataka Vijana wote waliopo katika vyuo vya VETA pamoja na Vituo vya ufundi stadi kuongeza maarifa zaidi ya ujuzi ili iwe rahisi kujiajiri na kufikia malengo yao.

Naye  mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa  ya Morogoro ambaye pia ndiye Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro, Chausiku Masegenya, amesema kuwa wamejipanga katika utoaji wa mafunzo katika vituo vyote vya ufundi vilivyopo Manispaa ya Morogoro katika kuwawezesha vijana kutimiza ndoto zao .

"Tumepokea maelekezo yote kutoka kwa Kiongozi wetu  Prof. Nombo ,  kulingana na ufinyu wa bajeti tulisuasua lakini tunaamini bajeti inayokuja licha ya mapungufu yaliyojitokeza , tutatenga bajeti kadri iwezekanavyo ili kuboresha miundombinu ya vituo vyetu vya ufundi Stadi , kama Manispaa  lengo letu kuona Vijana wanafanikiwa licha ya changamoto tulizonazo" Amesema Masegenya.

Kwa upande wa Mwalimu wa kituo cha ufundi stadi Shule ya Msingi Msamvu kitengo cha umeme , Mwl. Lidya Moleli , amempongeza Naibu Katibu Wizara ya Elimu kwa kufanya ziara katika kituo hicho pamoja na pongezi kwa Uongozi wa Manispaa na shule kwa jitihada mbalimbali wanazozifanya za kuhakikisha kituo hicho kinafanya kazi na Vijana wanajifunza taaluma zao licha ya changamoto zinazojitokeza.

Mwl. Moleli, amesema kuwa changamoto ni nyingi lakini wakitatuliwa changamoto za msingi kama vile vyumba vya madarasa pamoja ,  vifaa vya kujifunzia pamoja na Stoo za karakana wataweza kutoa elimu nzuri na Vijana wataelewa zaidi.

"Mimi mwalimu wa vitendo , wenzetu wa nadharia wakikosa nyanya ya kufundishia watachora hata ubaoni, sisi wa vitendo hatuwezi kuchora lazima tuwe na nyanya halisi ili tuweze kufundishia maana tukikosa dhana hiyo basi tutakuwa tunaharibu maana nzima ya dhana ya ufundi stadi  " Amesema Mwl. Moleli.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.