UWT CCM KATA YA MAFIGA WAMPONGEZA DIWANI KWA USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO.
Diwani wa Kata ya Mafiga Mhe. Thomas Butabile, akimkabidhi kiasi Cha Shilingi 50,000/= Mwenyekiti wa UWT Kata ya Mafiga, Salma Yange kwa ajili ya kufungua akaunti ya Benki ya mfuko wa Maendeleo kwa UWT Kata.
UMOJA wa Wanawake Tanzania ( UWT-CCM) Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro wamempongeza Diwani wa Kata ya Mafiga Mhe. Thomas Butabile kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya Maendeleo.
Pongezi hizo zimeongozwa na Mwenyekiti wa UWT Kata ya Mafiga, Salma Yange, leo Julai 10/2021 katika Mkutano wa UWT ulioambatana na Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo Kata ya Mafiga .
Akizungumza na Wajumbe wa UWT , Yange, amesema Diwani anafanya kile Wananchi walichomtuma na kutekeleza vyema Ilani ya CCM.
" Diwani wetu mchapa kazi, nampongeza Sana kwa usimamizi wake lakini pia shukrani kubwa kwa Mwanamke mwenzetu aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Dada yangu Sheilla Lukuba, kwa kweli ameacha alama kubwa Kama Mwanamke mwenzetu amethubutu na ameweza , lakini pia wataalamu wetu wa Manispaa na Kata na Wenyeviti wote wamefanya kazi kubwa kilichopo ni kuhakikisha kwamba tunailinda miradi hii kikamilifu ili iendeleee kuwahudumia Wananchi" Amesema Salma Yange.
Aidha, amewataka Wananchi wa Kata ya Mafiga waendelee kumuunga mkono Diwani kwani maendeleo makubwa yanatokana na nguvu za Serikali na Wananchi.
Pia ameupongeza miradi yote na kuiomba Serikali iendeleee kusaidia katika Maeneo mengine yenye uhitaji.
" Leo tulikuwa tunafungua Mkutano wetu wa UWT Kata, kwahiyo katika hilo tulimuomba Mhe. Diwani atupitishe katika miradi ili tupate sehemu ya kukisemea chama na kuona utekelezaji wa Ilani, miradi mizuri na thamani ya pesa imeonekana, tunampongeza Sana Diwani na wasaidizi wake , sisi tunaahidi tutashirikiana naye kikamilifu kuona Kata yetu inafikia malengo na Wananchi wanapata huduma bora" Amesema Salma Yange.
Naye Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe Thomas Butabile, ameishukuru UWT kwa ziara zao .
Butabile, amesema kuwa ataendelea kusimamia kikamilifu fedha za miradi zinazotolewa na Manispaa pamoja na nguvu za Wananchi ili ziwe na matunda.
" Tumefanya ziara na wenyewe Ilani wamejionea kwa kipindi kifupi yapo mambo ya kujivunia, niwaombe Sana Chama na Wananchi waendelee kutuunga mkono ili kazi iendeleee" Amesema Butabile.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa UWT Kata ya Uwanja wa Taifa ambaye alialikwa katika ziara hiyo, Zainabu Luimbo , amempongeza Diwani wa Mafiga kwa hatua za mwanzo ambazo amesema zinaonesha matumaini na mwanzo mzuri wa kuwatumikia Wananchi wake.
Naye , Fatuma Shomari,Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kidondoro B , amesema Wenyeviti wa Mitaa wamekuwa wakishirikiana bega kwa bega kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.
Hata hivyo, Katibu wa Wazee Kata ya Mafiga na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UWT , Bi. Mwanaidi Muhanga, amesema kwa niaba ya Kamati ya Utekelezaji na Baraza la Wazee wataendelea kumuunga Mkono Diwani na kuwa mstari wa mbele katika kufuatilia miradi iliyopo na ijayo.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa leo na UWT ni pamoja na Maabara ya Kituo Cha afya Mafiga, ujenzi wa Madarasa 4 na Ofisi za Waalimu Shule za Msingi Misufini B na Mafiga A, Ujenzi wa Madarasa 3 Shule ya Sekondari Mafiga na Jengo la Utawala, na ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Kata Mafiga.
Post a Comment