Header Ads

Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya siasa kuandaliwa


SERIKALI imesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, inaendelea kukusanya maoni ya wadau kwa lengo la kuandaa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992.

Hayo yalielezwa bungeni mjini hapa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasilisha hotuba yake kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inaendelea na mchakato huo ikiwa ni sehemu ya maadalizi ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992 pamoja na kanuni zake.

Alisema ofisi hiyo imeendelea kuhakikisha kuwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa inaimarika, katika mwaka huu wa fedha iliratibu kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa na ambacho mbali na kufanya uchaguzi wa viongozi wa baraza hilo, kilijadili mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria Mpya ya Vyama vya Siasa.

Wakati serikali ikiyasema hayo, Bunge limeitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutosita kukifutia usajili chama chochote kitakachokiuka sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyama vya siasa nchini.

Ofisi hiyo pia imetakiwa kusimamia na kuchunguza kwa ukaribu mienendo inayoharibu sifa na vigezo vya vyama vya siasa nchini.

Vilevile, Bunge limeitaka ofisi hiyo kufuatilia na kufanya ukaguzi wa matumizi ya ruzuku kwa vyama vya siasa ili kuhakikisha matumizi yao yanazingatia madhumuni yaliyokusudiwa.

Maagizo hayo yalitolewa bungeni mjini hapa jana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipowasilisha taarifa yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Akiwasilisha taarifa hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa, alisema chama husika kisipewe ruzuku tena endapo ikibainika ruzuku zinatumika tofauti na madhumuni yaliyokusudiwa.

Alisema hatua hiyo itatoa fundisho kwa vyama vya siasa kuzingatia matumizi stahiki ya fedha za wananchi.

"Kamati pia inashauri Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na weledi katika kusimamia utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa na kuhakikisha taratibu husika zinatumika katika utoaji ruzuku hizo," alisema.

Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji (CCM), alisema kamati yake inaendelea kuishauri ofisi hiyo kuchukua jitihada za kutosha kusuluhisha mgogoro katika Chama cha Wananchi (CUF) ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza katika muungano.

Akiizungumzia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mchengerwa alisema kamati inaitaka kuendelea kuboresha daftari la wapigakura na kuchukua jitihada za kutosha katika kuboresha daftari hilo.

"Hatua hizo zijumuishe utoaji elimu ya uraia hususan uandikishaji wa wapigakura kwa vijana ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga au kupigiwa kura," alisema na kuongeza:

"Hali hii itaongeza idadi ya Watanzania wengi zaidi wenye sifa na vigezo vya kupiga kura katika chaguzi mbalimbali zinazokuja."

Mwenyekiti huyo alisema tume inapaswa kujitahidi kufanyakazi kwa weledi, ili kuendelea kuaminika kwa wadau wa uchaguzi.

Pia alisema inapaswa kuhakikisha inawashirikisha wadau wa uchaguzi wakati wa uhuishaji wa daftari la wapigakura kuepuka migogoro isiyokuwa na tija kwa taifa.

"Kamati inashauri tume ihakikishe inawafuatilia wasimamizi wake wa uchaguzi na kuwawajibisha pale wanapofanya uzembe unaosababisha madhara yanayoweza kudhibitiwa," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, Oscar Mukassa, alisema matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo linaloongezeka kwa kiasi kikubwa.

Alisema serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mamlaka na wadau wanatoa elimu ya kutosha kwa jamii kufahamu madhara ya dawa za kulevya.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.