Header Ads

Mbaroni mwa Polisi kwa kuwachinja watoto wake

Respicius Diocress, mkazi wa kijiji cha Butayaibega wilayani Bukoba mkoani Kagera anatuhumiwa kuchinja kwa panga na kuwatenganisha kichwa na kiwiliwili watoto wake wawili mapacha.

Aidha, imeelezwa baada ya kuwachinja mapacha hao wenye umri wa miaka minne Diocress alimkabidhi mwanawe mkubwa, Japhet Respicius (5) Biblia ili awaombee marehemu kisha yeye kutoroka.

Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji hao, afisa mtendaji wa kijiji cha Butayaibega, Geofrey Deogratias alisema tukio hilo lilitokea saa saba usiku wa kuamkia Jumapili.

“Nilifika eneo la tukio na kukuta miili ya watoto Devotha Nyangoma Respicius (4) na pacha mwenzake Johanes Kato Respicius (4) ikiwa imelazwa sebuleni katika nyumba ya mtuhumiwa, huku vichwa vyao vikiwa pembeni mwa miili hiyo” alisema.

“Huyu mtuhumiwa alikuwa na watoto watatu ndani ya nyumba yake, lakini mtoto mmoja Japhet Respicius (5) hakumuua na alishuhudia baba yake akifanya unyama huo kwa wadogo zake.”

Mtendaji huyo alisema baada ya kuona hali halisi alipiga simu polisi kutoa taarifa juu ya tukio hilo, ambao walifika na kuichukua miili hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Alisema alipofika eneo la tukio alimkuta mtoto mkubwa akiwa nje ya nyumba akilia, na kuwaeleza kuwa baada ya baba yao kuwachinja wadogo zake alimkabidhi Biblia na kumsihi aendelee kuwaombea.

“Mtuhumiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo alitoroka na kuelekea kusikojulikana, lakini ameendelea kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa mwenyekiti wa kijiji, mtendaji na baadhi ya wanafamilia” alisema mtendaji Deogratias.

Alisema kuwa sehemu ya ujumbe huo ilisomeka: “Mwambie bibi Geogina ambaye ni bibi wa mke wangu aitwaye Kokwenda David kuwa nimekwishatekeleza alichokitaka kwa kuwaua Nyangoma na Kato, na mimi niko salama ila bado nawatafuta wengine wawili ili niwaue na kujipeleka polisi mwenyewe, msinitafute.”

Alisema baada ya polisi kuchukua miili ya marehemu hao, mtuhumiwa alirudi tena eneo la tukio akiwa na panga mkononi na kufyeka migomba yake na kuchoma nyumba yake moto, huku akiwatishia ndugu na jamaa zake kuwa wakimsogelea atawafyeka, na baadae alikimbia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Ollomi amesema baada ya msako mkali, mtuhumiwa ametiwa mbaroni   jana  Aprili 16  jijini Mwanza baada ya kutoroka na taratibu za kumsafirisha ili akabiliane na mashitaka zinafanyika.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.