TCRA imewapa wamiliki wa blogu Tanzania wiki mbili kujisajili
Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA ) imewapa muda wa wiki mbili wamiliki wa mitandao ya kijamii ya 'blogs', tovuti na aina nyingine ya vyombo vya habari vya habari vinavyochapisha kwenye mtandao kujisajili nchini Tanzania.
Hatua hii imekuja ili kudhibiti maudhui mitandaoni ikiwa ni matakwa ya sheria mpya ambayo ilionekana kuwa na mkanganyo.
Ikiwa sehemu ya usajili, wachapishaji wote wa kwenye mtandao kwa maandishi, video na sauti wanapaswa kulipa dola 1000.
Aidha wachapishaji wa mtandao huo wanatakiwa kuhakikisha wanakamilisha vigezo vyote ambavyo wanatakiwa kuainisha ikiwa ni pamoja kuweka mfumo wakukagua taarifa zisozoruhusiwa katika mitandao na kuweka rekodi ya watumiaji wote, vikiwemo vitambulisho vyao na anuani za wasambazaji wa intaneti.
Atakaye kiuka vigezo muhimu vilivyowekwa atapata adhabu ya kulipa faini isiyopungua dola 2000 au kufungwa jela kwa muda usiopungua mwaka mmoja au adhabu zote kwa pamoja.
Wanaharakati wengi, watumiaji wa mtandao na wamiliki wa mitandao hiyo wameona serikali imeamua kutumia mwanya huo ili kubana uhuru wa kujieleza.
Lakini serikali ya Tanzania inasema imeamua kuchukua maamuzi hayo ili kulinda taifa na maudhui kutoka nje au ndani ya nchi ambayo hayahitajiki katika jamii.
Hata hivyo mwenyekiti wa wamiliki wa blogu ndugu Johakimu Mushi anasema wao kama Tanzania bloggers hawana tatizo kabisa na suala la kujisajili maana wanajua umuhimu wa kusajiliwa ni kuonekana kwamba wanatambuliwa na kazi wanazozifanya na itasaidia kuangalia maadili.
Changamoto iliyopo kwa wamiliki hao wa mitandao wanasema inakuja kwenye ulipaji wa tozo
"suala tata ni kuhusiana na tozo zilizowekwa maana sio bloggers wote wanafanya biashara sana kuna wengine wanatoa elimu tu ya afya au michezo na hakuna faida yeyote wanayopata hivyo itakuwa ngumu kwa wao kuendelea kuchapisha kwenye mtandao,tunataka kutoa ushirikiano wa dhati lakini kiuhalisia ni ngumu hivyo inabidi TCRA watoe elimu kwanza,"Jonathan aeleza.
Post a Comment