Hospitali za rufaa kufungwa X-ray za kidigitali
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imepanga kuleta mashine 34 za kisasa za X-Ray za kidigitali ambazo zitafungwa kwa Hospitali za rufaa za mikoa yote.
Hayo yalibainishwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Faustine Ndungulile, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Jasmine Tisekwa.
Tisekwa alitaka kujua ni lini serikali itapeleka X-ray ya kisasa ya kidigitali katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ili kuondokana na adha kubwa wanayoipata wagonjwa kwa kuwa ile ya zamani ni chakavu.
Akijibu swali hilo, Dk. Ndungulile alisema mashine hizo zitaletwa na kampuni ya Philips ambayo ina mkataba wa matengenezo wa mwaka 2012/16 ambao unalenga kufanya matengenezo na kuzibadilisha mashine chakavu na kuweka mpya.
Alibainisha mashine hizo zitafungwa katika mikoa yote nchini ikiwemo hospitali ya rufani ya mkoa na awamu ya kwanza ya kuletwa kwa mashine inatarajiwa kuwa Juni, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema wizara inatambua umuhimu wa huduma za uchunguzi wa kutumia mionzi ya radiolojia na inatambua changamoto ya uchakavu wa mitambo hiyo.
Aidha alisema gharama kubwa ya matengenezo inayoathiri upatikanaji wa huduma hiyo katika mwaka wa fedha 2017/18.
“Ili kukabiliana na gharama kubwa za kununua na kufanya matengenezo ya vifaa vya uchunguzi, wizara imeanza kufanya uchambuzi ikiwa ni pamoja na kuangalia uzoefu wa nchi zingine ambazo zilishaanza kutumia utaratibu wa kukodisha vifaa na kulipia huduma,”alisema.
Naibu Waziri huyo alisema Wizara inatarajia kutumia uzoefu huo kuandaa miongozo itakayowezesha kutekelezwa kwa utaratibu huo kwa ufanisi.
Post a Comment